Watu
watatu wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa baada ya gari aina
ya Toyota Noah kugongana na lori eneo la Ubena Zomozi mkoani Pwani
usiku wa kuamkia leo.
Naibu
mkurugenzi wa ulinzi na usalama wa CUF, Masoud Mhina akizungumzia ajali
hiyo, amesema waliokufa ni wanachama wa chama hicho mkoani Tanga.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga amesema ajali hiyo ilitokea saa
8:30 usiku wa kuamkia leo Septemba 6 baada ya Toyota Noah lililokuwa
likitokea Dodoma kuhama njia na kugongana na lori.
Lyanga amesema lori hilo lilikuwa likiendeshwa na Yassin Hamad mkazi wa Dar es Salaam.
Amesema
waliokufa katika ajali hiyo ni Uledi Salumaa (32) ambaye alikuwa dereva
wa Toyota Noah, Mary Komba (40) na mwingine aliyetambuliwa kwa jina
moja la Isack, wote wakazi wa Muheza mkoani Tanga.
Kamanda
Lyanga amewataja majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Juma Nindi, Chausiku
Hassan na Esther Masie ambao pia ni wakazi wa Muheza.
Amesema
miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Tumbi mjini Kibaha
na majeruhi walipelekwa kwa matibabu katika Kituo cha Afya Chalinze.
Kamanda Lyanga ametoa wito kwa madereva kuacha kuendesha kwa mwendo wa kasi na hasa usiku kwa kuwa madhara yake huwa makubwa.
“Niwatake
madereva wote wanaoendesha magari usiku, ukijihisi umechoka weka gari
pembeni pumzika. Ukilazimisha utakuwa kama huyu ambaye alihama upande
wake na kugongana na lori,” amesema.
No comments:
Post a Comment