kimataifa

Hair Food

TANGAZO

TANGAZO

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, 3 May 2016

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu Atoa ONYO Kali kwa Wanaume Wanaowapa Mimba Wanafunzi


Serikali imewaagiza Maafisa maendeleo ya Jamii na maafisa ustawi wa Jamii wa wilaya,kata na mikoa nchini kuwafatilia wanaume wanaowapa ujauzito watoto wa shule na kuwafikisha Mahakamani.

Akizungumza leo bungeni katika kipindi cha maswali na majibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu, amesema serikali haitamvumilia mwanaume yoyote anaempa mwanafunzi ujauzito.

Mhe. Ummy amesema kuwa serikali ya awamu ya tano itawachukulia hatua wanaume wote na hakutakuwa na huruma juu ya hilo huku akisisitiza wanawake ambao si wanafunzi ni wengi mitaani.

Hapo awali Akijibu Swali la Mbunge wa Ileje, Mhe. Janeth Mbene, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Seleman Jaffo amesema kuwa tatizo la watoto kupewa ujauzito nchini linatokana na vishawishi wanavyokutana wakiwa njiani wakati wanakwenda mashuleni.

Sumaye Ampiga Kijembe Rais Magufuli


FREDERICK Sumaye, Waziri Mkuu Mstaafu ameeleza kushangazwa na Serikali ya Rais John Magufuli kupenda kusifiwa zaidi na kuchukia kukosolewa

Sumaye bila kumtaja jina Rais Magufuli ameleza kushangazwa na hatua ya serikali kuminya uhuru wa habari na kwamba, kufanya hivyo kunalenga kuficha madudu yanayofanywa na watendaji wake.

“Wapowatawala ambao hawapendi kusemwa lakini wanapenda sana kusifiwa. Kiongozi mwenye tabia ya udikteta hataki kusikia kingine zaidi ya sifa zake tu.

“Huyo ni mtu hatari na katika nchi ya namna hiyo hakuna uhuru wa habari wala uhuru wa kutoa maoni kwa woga wa kupotezwa kusikojulikana,”amesema Sumaye.

Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliyoratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habri za Siasa (TAPOREA), Sumaye amesema, serikali inakiuka Katiba ya nchi.

Amesema, serikali yoyote inayopambana na vyombo vya habari na kuminya uhuru wa kufanya kazi zao huwa ina tatizo kwa upande wa wanaotawala.

Akitolea mfano wa hatua ya serikali kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya bunge Sumaye amesema, kwa kufanya hivyo serikali imevunja Katiba.

“Unapoondoa matangazo ya moja kwa moja ya vipindi vya Bunge, kwanza ni kuvunja katiba. Ibara ya 18 (d) ya Katiba inasema, kila mtu ana haki ya kupewa taarifa wakati wote.

“Kwa kuzuia Bunge kuoneshwa ‘live’ (moja kwa moja) wewe serikali unataka kutoa taarifa ya Bunge kwa wakati unaoutaka na kwa taarifa unayoitaka wewe,” ameeleza Sumaye.

Kuhusu sababu iliyotolewa kwamba, matangazo hayo yanatumia gharama ya Sh. 4 bilioni amesema haina mashiko.

Sumaye amesema, hata kama matangazo hayo yatarushwa na ofisi za bunge bado, gharama zitaongezeka zaidi kwa sababu Bunge litahitaji kununua mitambo pamoja na kuajiri wafanyakazi wake.

Sumaye amesema, serikali yenye demokrasia ya kweli lazima ikubali wananchi wake kutoa maoni.

“Serikali yoyote yenye utawala bora, ingependa mambo yake inayoyafanya kwa ajili ya wananchi wake mambo hayo yajulikane kwa wananchi hao.

“Ukiona serikali inaficha mambo yake lazima kuna mambo wanayoyafanya ambayo hayafai na wasingependa jamii ijue,” amesema Sumaye.

George Maziku, Mkurugenzi Mtendaji wa TAPOREA amezungumzia ripoti ya hali ya uhuru wa waandishi wa habari na uhuru wa vyombo vya habari kimataifa, iliyotolewa na Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka lenye Makao Makuu yake nchini Ufaransa haipendezi.

Amesema, ripoti hiyo inaonesha kuwa, katika miaka 10 iliyopita zaidi ya waandishi wa habari 800 kutoka mataifa mabalimbali duniani wameuawa wakiwa wanatekeleza kazi zao.

“Kitisho kingine kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini ni utamaduni mpya ulioasisiwa na kuimarishwa na watawala wa sasa na kuvishinikiza vyombo vya habari kutomkosoa Rais John Magufuli na serikali yake.

“Matokeo yake, vyombo vingi vya habari nchini vimelazimika kuandika habari za kumfurahisha Rais Magufuli,” amesema Maziku.

Monday, 2 May 2016

Watahiniwa 75,000 Waanza Mtihani wa Kidato cha Sita Leo


Watahiniwa  74,920 leo wanaanza kufanya mtihani wa kuhitimu Kidato cha Sita katika shule mbalimbali nchini huku watahiniwa 11,597 wakifanya mtihani wa Ualimu.

Ofisa Habari wa Baraza la Mitihani (NECTA), John Nchimbi amesema kuwa mtihani wa kidato cha sita unaanza leo hadi Mei 19, mwaka huu. 

Nchimbi amesema kati ya watahiniwa hao waliosajiliwa, watahiniwa 65,610 ni watahiniwa wa Shule huku watahiniwa wa Kujitegemea wakiwa 9,310.

“Kati ya watahiniwa wa shule 65, 610, watahiniwa wasichana ni 24,549 na wavulana ni 41,061 huku watahiniwa wa kujitegemea wasichana wakiwa ni 3,176 na wavulana ni 6,134,” alisema Nchimbi.

Kwa upande wa mtihani wa ualimu, Nchimbi amesema kati ya watahiniwa 11,597 watakaofanya, watahiniwa 10,942 wanafanya Ualimu Daraja A na watahiniwa 654 wanafanya mtihani wa Stashahada ya Sekondari na mmoja anafanya Stashahada ya Ufundi.

“NECTA inatoa mwito kwa kamati za mitihani za mikoa, na wilaya kuhakikisha kuwa taratibu zote za mitihani zinazingatiwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mazingira ya vituo vya mitihani yapo salama, tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha udanganyifu. 

“Kwa wanafunzi tunaamini walimu wamewaandaa vizuri, na ni matarajio yetu wanafunzi watafanya mitihani yao kwa kuzingatia taratibu zote za mitihani ili matokeo ya mitihani yaoneshe uwezo wao halisi kulingana na maarifa na ujuzi waliopata katika kipindi walipokuwa shule,” aliongeza Nchimbi.

Aidha, Nchimbi alitoa mwito kwa jamii kutoa ushirikiano unaotakiwa kuhakikisha mtihani unafanyika kwa amani na utulivu na kusisitiza kuwa mtu asiyehusika na mtihani asiingie kwenye eneo la mtihani.

Mchakato wa kumkabidhi Rais Magufuli Uenyekiti wa CCM waanza


Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), inatarajiwa kukutana kesho mjini Dodoma.

 

Chanzo cha kuaminika kimedokezakuwa pamoja na mambo mengine, kikao hicho kitajadili maandalizi ya mkutano mkuu maalumu, ambao unatarajiwa kufanyika Juni mjini hapa.

 

Kwamba katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ataachia ngazi na kumkabidhi Rais Dk. John Magufuli kama utamaduni wa chama hicho ulivyo katika kukabidhiana kijiti cha uongozi.

 

Tangu wiki iliyopita vikao kadhaa vya Sekretarieti vimekuwa vikiendelea mjini hapa, vikiwahusisha watendaji wa juu wa CCM pamoja na makatibu wa idara husika ambao huteuliwa na mwenyekiti kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

 

Kikao hicho cha kesho pia kinatarajiwa kuhudhuriwa na Rais Magufuli, ambaye tayari yupo mjini hapa alipokuja kwa ajili ya sherehe za Sikukuu ya Wafanyakazi – Mei Mosi.

 

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa nao wataungana na viongozi wa ngazi za juu wa CCM katika kikao hicho.

 

Katika kikao cha kesho, Kamati Kuu pia itajadili na kupitisha majina ya wajumbe 10 wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), kutoka miongoni mwa wabunge wa CCM.

 

Habari kutoka ndani ya chama hicho zilieleza kuwa kikao hicho kitakuwa chini ya Mwenyekiti wake Kikwete, ambapo wabunge walioomba nafasi hizo, majina yao yatapelekwa kwa wabunge wa chama hicho kwa ajili ya kupigiwa kura.

 

“Wabunge wana nafasi 10 za NEC na unajua waliokuwa wajumbe walishapoteza sifa za kuwa wajumbe, hivyo kwa kawaida kila Bunge jipya linapochaguliwa ni lazima uchaguzi ufanyike.

 

“Pamoja na kupitia majina ya wabunge waliojaza fomu, pia CC itajadili majina ya wabunge walioomba nafasi ya katibu wa wabunge wa CCM ambapo kuna wajumbe zaidi ya watatu wamejaza fomu,” kilisema chanzo hicho.

 

Kwa mujibu wa chanzo hicho, miongoni mwa wabunge wanaotajwa kuwania nafasi ya katibu wa wabunge wa CCM yumo Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda, ingawa wapo wabunge wengine ambao kwa pamoja watachujwa na kikao cha kesho.

 

Katibu wa Kamati ya Wabunge wa CCM anayemaliza muda wake ni Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama.

Taarifa Kwa Umma Kutoka Makao Makuu Ya JKT

Picha: Nyumba 400 Zabomolewa Eneo la Iloganzila Jimbo la Kibamba Jijini Dar es Salaam

Wakazi waliojenga eneo la Iloganzila Jimbo la Kibamba Dar es salaam leo wamebomolewa nyumba zao ambazo ni zaidi ya nyumba 400, zoezi hilo limekuja baada ya amri iliyotolewa na Mahakama Kuu juzi.

Taarifa zinasema eneo hilo lenye ukubwa wa heka 33, mali ya Henry Kashangaki lilikuwa na mgogoro tangu 1997 baada ya kundi la watu 11 kuvamia na kuanza kujenga nyumba na kuwauzia wananchi wengine.

Baada ya eneo hilo kuvamiwa mmiliki wake aliamua kwenda mahakamani na kuwashtaki Shaha Matibwa na wenzake kumi, kesi hiyo iliendeshwa kwa muda wa miaka mitano na mwaka 2010 hukumu ilitolewa na Kashangaki na Matibwa walionekana wana haki ya kumiliki hivyo walitakiwa kugawana.

Hata hivyo, Kashangaki hakuridhika na hukumu hiyo na kukata rufaa na kwenda Mahakama Kuu, January 2016 kesi hiyo ilitolewa hukumu na Kashangaki alishinda, hivyo juzi Mahakama hiyo ilitoa amri nyumba zivunjwe ili kumpisha mwenye eneo lake.

Askari wa Usalama Barabarani Aliyetukanwa na Mke wa Waziri Apandishwe Cheo

Rais John Magufuli ameagiza Koplo Deogratius Mbango kupandishwa cheo baada ya kumdhibiti mke wa waziri mmoja wa Serikali yake aliyepambana na askari huyo wa barabarani baada ya dereva wake kufanya kosa eneo la Namanga jijini Dar es Salaam.

Koplo Mbango alikumbana na tukio hilo baada ya dereva wa mke huyo wa waziri kusimama kwenye alama za kuruhusu watembea kwa mguu kuvuka barabara na alilazimika kupiga simu kituoni kupata maelekezo baada ya mama huyo kujitambulisha kuwa ni mke wa waziri.

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha kazi cha makamanda wa polisi wa mikoa, mawakili wafawidhi wa Serikali, na wakuu wa upelelezi wa mikoa na vikosi, kilichofanyika mjini Dodoma, Rais Magufuli bila kumtaja jina alisema amemwonya waziri huyo na mkewe.

“Ebo! Yule trafiki anajua kazi, mpandishe cheo. Na huyo waziri na mke wake nimeshamwambia,” alisema Rais Magufuli, kwa mujibu wa taarifa ya habari ya TBC1.

Licha ya polisi na Rais Magufuli kutotaja jina la waziri huyo, mazungumzo kwa njia ya simu ambayo yamesambaa yanaonyesha mwanamke huyo aliyekamatwa akijitambulisha kwa jina la waziri mmoja mpya katika Serikali ya Awamu ya Tano.

Majibizano ya polisi na mama huyo yanaonyesha kuwa dereva wake alikamatwa baada ya kusimama katikati ya mistari ya pundamilia, ambayo ni ishara ya kuvukia waendao kwa miguu.

Mazungumzo hayo yaliyorekodiwa yanaanza wakati Koplo Deogratius alipompigia simu kamanda wa trafiki wa Kinondoni, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Awadh Haji na kumueleza tukio lililokuwa mbele yake.

Kadhalika Koplo Deogratius alimueleza RTO Haji kuwa wakati anataka kumuandikia faini, dereva huyo alitaka kuondoa gari na mama huyo akamtukana.

“Huyu mama akawa ananitukana… anasema yeye ni mke wa waziri. Nikamuambia hilo ni kosa la dereva, hivyo sitaruhusu aondoke bali nitampeleka kituoni. Wakati namuamuru dereva aende kituoni, akataka aondoke, nikamnyang’anya funguo ili nimpeleke kituoni,” alisema Koplo Deogratius.

“Ameniita mimi mshenzi, sina akili. Anasema yeye ni mke wa waziri gani?.. Anasema yeye sijui mke wa waziri (anamtaja jina).”

Baadaye Kamanda Haji anataka aongee na mama huyo ambaye mazungumzo yanaonyesha anakanusha kumtukana askari huyo, akisema alikuwa akimuomba amuelimishe dereva kwa kuwa kosa alilofanya ni dogo.

“Mimi sikumtukana, wala sikumwambia maneno hayo namshangaa sijui leo ameamkaje. Kitu nilichomuambia kwamba huyu kijana (dereva) alikuwa anakwenda moja kwa moja, mimi nilikuwa na vihela kidogo nilikuwa nataka kuchenji ili nimpe fundi,” alisema mke huyo wa waziri.

“Nikauliza kosa gani, akasema eti kosa lake ni kusimama kwenye zebra crossing. Nikamuambia sawa, hilo ni kosa la kuelimishwa, lakini sasa wewe unamuandikia kwa kosa kama hilo? Hilo ni kosa dogo, very minor la kuweza kumuandikia? Lakini kama unamuandikia andika.” 

Kupitia maongezi hayo, RTO Haji alisema kosa hilo ni kubwa na lina adhabu kali.

“Nikusaidie kitu kimoja, katika makosa mabaya sana mojawapo ni dereva kutoheshimu zebra crossing. Mahakama inapomkuta mtu na hatia ya kugonga kwenye zebra crossing, adhabu yake ni jela miezi sita. Haina hata faini, hiyo tunaita dangerous driving (uendeshaji wa hatari),”alisema Haji na kumtaka Koplo Deogratius kumuadhibu dereva kwa kosa lake.

Alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo, Koplo Deogratius alikiri kupambana na mke huyo wa waziri, lakini hakutaka kuingia kwa undani akisema yeye si msemaji wa Jeshi la Polisi.

“Ni kweli nilimkamata huyo mama lakini, kwanza tuelewane. Mimi siyo msemaji wa polisi. Kama unataka kesho uje pale kituoni, umuone RTO. Kama akiruhusu mimi nitaeleza kila kitu,” alisema Deogratius akiwa maeneo ya Namanga. 

Naye Kamanda Haji alithibitisha tukio hilo, lakini akamuelekeza mwandishi kumuuliza kamanda wa polisi mkoani Kinondoni, Christopher Fuime.

Kamanda Fuime alisemai kuwa Rais Magufuli ameagiza koplo huyo apandishwe cheo kutokana na kusimamia sheria na kwamba agizo hilo linafanyiwa kazi.

“Mimi ndiyo natoka Dodoma kwenye hicho kikao cha Rais na maofisa wa polisi. Hilo ni agizo, sasa unataka tulipinge? Hayo ni mambo ya utawala, wataangalia wenyewe kama apewe cheo gani. Kwa sasa yeye ni Koplo, kwa hiyo watajua wenyewe wampe nini. Afande IGP ndiyo anajua,”alisema Fuime.

There was an error in this gadget