Tuesday 22 January 2013

AFYA YA DCI MANUMBA YAANZA KUIMARIKA, BADO TUPO KATIKA CHUMBA MAALUMU CHA UANGALIZI (ICU) CHINI YA MADAKTARI NA WAUGUZI HOSPITALI YA AGA KHAN.



DCI ROBERT MANUMBA.

UONGOZI wa Hospitali ya Aga Khan inayompatia matibabu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Nchini (DCI), Robert Manumba, ambaye amelazwa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU), umesema hali ya mgonjwa wao inaendelea kuwa ya kuridhisha na anaendelea na matibabu chini ya madaktari na wauguzi.

Uongozi huo licha ya mwishoni mwa wiki iliyopita kuahidi kuzungumza na waandishi wa habari jana, ulishindwa kufanya hivyo na badala yake ulitoa taarifa kwa maandishi kuelezea maendeleo ya afya ya Manumba.

“Manumba bado anaendelea na matibabu na hali yake ni ya kuridhisha. 

Alifikishwa hospitalini Januari 15, kwa tatizo la malaria kali iliyoathiri viungo vya mwili,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Daktari mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Jaffer Dharsee, hakuwa tayari kueleza zaidi juu ya hali ya mgonjwa huyo, huku akiwataka waandishi kuwa na subira, kwani watakuwa wakipatiwa taarifa kwa maandishi.

“Hali inaendelea vizuri na tutakuwa tunawapatia taarifa kila siku mchana; tunaomba ushirikiano wenu,” alisema Dk. Dharsee alipozungumza na waandishi wa habari.

Ulinzi katika hospitali hiyo umeimarishwa kutokana na viongozi mbalimbali kufika hospitalini hapo kumjulia hali Manumba.

No comments: