Tuesday 22 January 2013

TUNDU LISSU: ZIMEBAKI DAKIKA 5 KUING'OA CCM MADARAKANI







Mbunge wa Singida  Mashariki kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema ) na mnadhimu mkuu wa Kambi ya upinzani bungeni Mh.Tundu Lissu amesema kuwa Chadema haiwezi kuishinda na  kuiondoa  CCM madarakani kwa  maneno tu, bali ni kuwakaba na kwenda nao bega kwa bega, mtu na mtu, hatua kwa hatua na kuhakikisha ushindi wa 2015 upo mikononi mwao.
 Lissu aliyasema hayo juzi jijini Dar es salaam katika Viwanja vya Buibui  alipokuwa akizindua matawi  Malongwe na Kambangwa katika  jimbo la  kinondoni kata ya Mwananyamala na kusaini kadi  70 za wanachama wapya ikiwa ni  moja ya vuguvugu la mabadiliko na kujizatiti kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Alisema kuwa  zimebaki  dakika tano tu wananchi kuamua, kujipanga na kuwajibika katika kuing’oa CCM madarakani,  kwa sababu hakuna mkataba  unaowalazimisha  wananchi kuumia nakuteseka  katika  maamuzi na  matumizi ya  rasilimali zao.
“Kama mpira umefikia dakika ya 85 bila ushindi hivyo tuna dakika 5 tu kupigana na kuhakikisha tunawashinda wapinzani bila kujali na kulazimishwa kuwa watumwa katika nchi yetu wenyewe, ”Alisema Lissu.
Alisema kuwa lengo la  Chadema ni  kurudisha serikali mikononi mwa  Umma ikiwa tu  wataamka na kuiunga mkono chadema   na kudai kuwa mabadiliko yapo mikononi mwa wananchi na uwajibikaji wao ili kufikia malengo.
“CCM itaondolewa madarakani kwa watu wanaoweza kuwajibika ipasavyo, mwanzo tulishindwa kwa sababu hatukuwajibika sawasawa na hatukuwa makini na  kura zilizopigwa lakini sasa tupo makini ,tume jipanga ili kuhakikisha  safari hii  ushindi ni wetu”, Alisema Lissu.
Nae Mbunge wa Ubungo Mh. John Mnyika alisema kuwa kushindwa kwa CCM kuteteleza matakwa ya wananchi ni wazi kuwa wameshindwa kuongoza hivyo ni vyema wakaachia madaraka kwa vyama vingine na sio kung’ng’ania madaraka ikiwa wameshindwa kuifikisha nchi mahali stahiki na wananchi kunufaika na nchi yao, hivyo wananchi wasikubali kudanganywa tena na CCM .
“Tunahitaji kufanya madiliko kwa sababu mwaka  2005 CCM  waliahidi  wataleta maisha bora kwa kila Mtanzania, Ajira kwa vijana kwa wingi kwa kauli mbiu yao ya Ari mpya, Nguvu mpya  na Kasi mpya wakapita lakini  bado hali ilikuwa ni ngumu isiyoelezeka, ilipofika 2010 wakaja na kauli mpya iliyosema Ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi ambayo sasa imeleta hali ngumu zaidi, ”Alisema Mnyika.
Nae mmoja kati ya wenyeviti waliosimikwa Francis Nyerere Tawi la Kambangwa, alisema kuwa wamechoshwa na mambo  yanayofanywa na chama tawala katika mgawanyiko wa utendaji kazi usiowanufaisha wananchi.

“Miundo mbinu inatengenezwa na kurekebishwa  pale zinzpojitokeza shughuli maalum za kiserikali kama mbio za mwenge kitu ambacho kimenifanya  nijiiulize kipi bora kati  ya wananchi na mwenge ili kumpa thamani mwananchi wa hali ya chini  ambaye hakumbukwi mpaka  zitokee shughuli kama hizi”, Alisema Nyerere.

No comments: