Tanzania
(Taifa Stars) imeshindwa kufuzu Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani
(CHAN) kwa mara ya pili mfululizo baada ya leo (Julai 27 mwaka huu)
kufungwa mabao 3-1 na Uganda Cranes, hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao
4-1.
hdg
Stars
ambayo ilicheza fainali za kwanza zilizofanyika Ivory Coast mwaka 2009
ilimaliza kipindi cha kwanza katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa
Taifa wa Mandela ulioko Namboole nje kidogo ya Kampala ikiwa sare ya bao
1-1.
Wenyeji
ndiyo walioanza kufunga bao dakika ya saba katika mechi hiyo
iliyochezeshwa na Kanoso Abdoul Ohabee kutoka Madagascar. Frank Kalanda
alifunga bao hilo akimalizia mpira uliopigwa ndani ya eneo la hatari la
Tanzania.
Bao hilo
halikuonekana kuichangaza Taifa Stars, kwani ilitulia na kufanikiwa
kusawazisha dakika ya 18 mfungaji akiwa Amri Kiemba kutokana na pasi
nzuri ya Mrisho Ngasa kwenye kona ya eneo la mita 18.
Dakika ya
32 nusura Taifa Stars ipate bao, lakini mkwaju maridadi wa Mrisho Ngasa
ambao tayari ulikuwa umempira kipa HAmza Muwonge uligonga mwamba kabla
ya kuokolewa na mabeki wa Uganda Cranes.
Mabao
mengine ya Uganda Cranes yalifungwa dakika ya 48 kupitia kwa Brian
Majwega na lingine dakika ya 63 mfungaji akiwa tenda Kalanda kutokana na
makosa ya Salum Abubakar kupokonywa mpira wakati akiwa katika nafasi
nzuri ya kutoa pasi kwa mwenzake.
Kocha Kim
Poulsen alifanya mabadiliko dakika ya 43 kwa kumuingiza Simon Msuva
badala ya Frank Domayo aliyeumia, na dakika ya 78 akawaingiza kwa mpigo
Haruni Chanongo na Vincent Barnabas badala ya David Luhende na John
Bocco. Hata hivyo mabadiliko hayo hayakubadili matokeo ya mchezo.
Kikosi
cha Stars kilipangwa hivi; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, David
Luhende/Vincent Barnabas, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Athuman Idd,
Frank Domayo/Simon Msuva, Salum Abubakar, John Bocco/Haruni Chanongo,
Amri Kiemba na Mrisho Ngasa.
Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itarejea nyumbani kesho
(Julai 28 mwaka huu) saa 4 usiku kwa ndege ya PrecisionAir.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment