Afisa Elimu-Sekondari wa Wilaya ya Temeke Bwana Donald Chavila
Meneja Uragibishi na Mawasiliano wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo, WAMA, Ndugu Philomena Marijani (aliyesimama)akitoa maelezo mafupi kuhusu semina ya siku 5 kwa wanafunzi wa Shule za Sekondari katika Wilaya ya Temeke itayozungumzia uzuiaji wa mimba za utotoni kwa wanafunzi wa wilaya hiyo. Semina hiyo inafanyika katika Shule ya Sekondari Kibasila kuanzia tarehe 13 hadi 17.4.2015.
Baadhi ya wanafunzi na walimu kutoka Shule 11 za Sekondari katika Wilaya ya Temeke wakisikiliza hotuba ya mgeni rasmi, Afisa Elimu-Sekondari wa Wilaya ya Temeke Ndugu Donald Chavila (hayuko pichani) wakati alipokuwa akifungua rasmi semina ya siku tano inayozungumzia uzuiaji wa mimba za utotoni kwa wanafunzi wa Wilaya hiyo tarehe 13.4.2015 kwenye ukumbi wa sherehe wa Kibasila Sekondari.
Na Anna Nkinda – Maelezo
Kuwepo kwa sheria na sera katika shule za msingi na Sekondari na kutoa elimu kwa wanajamii hasa wazazi na walezi kutapunguza mimba za utotoni zinasababisha vijana wa kike kushindwa kuendelea na masomo, kupoteza maisha yao na watoto watakaowazaa.
Hayo yamesemwa na Afisa Elimu Sekondari wilaya ya Temeke Mwalimu Chavila Donald wakati akifungua mafunzo ya elimu ya afya ya uzazi, ujinsia na stadi za maisha kwa wanafunzi na walimu wa shule za Sekondari za wilaya hiyo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa shule ya Sekondari Kibasila.
Mwalimu Chavila alisema wanafunzi ni watu wa muhimu wanategemewa katika familia, jamii na taifa katika kuleta maendeleo na kupunguza umaskini. Pamoja na changamoto wanazozipata bado wanawajibu wa kujilinda na kujitunza ili waweze kufikia ndoto zao.
"Kitu kikubwa mnachotakiwa kikifanya ni kusoma kwa bidii na kufanya vizuri katika masomo yenu ili muweze kuleta tofauti katika jamii pamoja na kuwa na maisha bora na kujiwekea misingi imara ya maisha ya baadaye", alisema Mwalimu Chavila.
Kwa upande wa walimu aliwahimiza kuwa msaada wa kitaaluma na kijamii kwa wanafunzi na kuhakikisha watoto wanapata elimu bora itakayowakwamua kifikra, kijamiii na kiuchumi.
Alisisitiza , "Elimu ndiyo silaha na nyenzo pekee ya kusukuma maendeleo ya watu na ya vitu kwa Dunia ya leo. Fikirieni na toeni mapendekezo ya jinsi ya kuishi kwenye ulimwengu wa utandawazi, hata kama italazimu kurekebisha mitaala ili iendane na matakwa ya mazingira haya mapya".
Naye Meneja Uraghibishi na Mawasiliano kutoka Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Philomena Marijani alisema mafunzo hayo ya siku tano yako chini ya mradi wa kuzuia mimba za utotoni katika shule za sekondari unaotelelezwa na Taasisi hiyo na Engender health kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la watu wa Marekani.
Aliyataja malengo ya mradi kuwa ni kuimarisha uelewa na ujuzi kuhusu afya ya uzazi kwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 14-19,kuongeza uhusishwaji na ushiriki wa wazazi , walezi, walimu na jamii kupinga mimba za utotoni na maambukizi ya Ukimwi kwa vijana na kufanya uraghibishi wa uelewa kwa njia za uzazi wa mpango ambazo zitasaidia kupunguza vifo vya akina mama na mimba zisizotarajiwa.
Philomena alisema, "Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika mradi huu ni shule za Sekondari 40 zimepata mafunzo ya afya ya uzazi na stadi za maisha ambayo yatamsaidia mtoto wa kike kujikinga na mazingira hatarishi pamoja na kufanya vyema katika masomo yake na kujiwekea malengo, klabu 40 zenye jina la jilinde utimize ndoto yako za uelimishaji rika na stadi za maisha zimeanzishwa".
Mikutano minne ya uhamasishaji jamii yenye lengo la kuwaelewesha wanajamii wajibu wao katika kuwalinda watoto wa kike na mimba za utotoni iliweza kufanyika na klabu 20 za kijamii zilizojumuisha wazazi, wasanii, waandishi wa habari na viongozi wa dini zenye jina la wote tunawajibu wa kuleta mabadiliko katika jamii zilianzishwa".
Aidha Afisa Miradi kutoka Engender health Dkt. Martha Kisanga aliwapongeza wanafunzi hao pamoja na walimu kwa kuwa miongoni mwa watu waliohudhuria mafunzo hayo ambayo yatawasaidia kupata elimu ya afya ya uzazi, ujinsia na stadi za maisha.
"Msikilize kwa umakini yale yote mtakayofundishwa kwani baada ya hapa mtakwenda kutoa elimu kwa wenzenu mliowaacha shuleni ili nao waweze kujiamini na kujua haki zao za msingi ikiwemo haki ya uzazi kwa kijana", alihimiza Dkt.Martha.
Mradi wa kuzuia mimba za utotoni katika Shule za Sekondari ulianzishwa mwaka 2010 -2012 na kufanyika katika mkoa wa Lindi kwenye wilaya za Lindi vijijini na Kilwa, Mkoa wa Mtwara katika wilaya za Nanyumbu na Masasi na mwaka 2014-2015 mradi unatekelezwa katika mkoa wa Dar es Salaam wilaya ya Temeke
No comments:
Post a Comment