Wednesday 13 August 2014

ACT YAKWAMA MBEYA



Na Christopher Nyenyembe- Tanzania DAIMA

CHAMA cha siasa cha ACT-Tanzania kimeingia kwenye anga za CHADEMA Mbeya na kujikuta kikipoteza kadi zaidi ya 100 kilichowashawishi wanachama wa CHADEMA ambao baada ya kuzipokea, zilitupwa usiku nje ya ofisi hizo.

Kadi za ACT, zilipatikana jana majira ya asubuhi na kusababisha uongozi wa CHADEMA Wilaya ya Mbeya, ukutane haraka katika ofisi hizo na kuzionyesha hadharani.

Kiongozi wa ulinzi na usalama wa CHADEMA Mbeya Mjini, Jamal Juma, alisema kuwa kadi, bendera na vipeperushi hivyo, vilikutwa nje ya ofisi hizo na alijulishwa haraka na wasaidizi wake kuwa wameokota nyaraka za ACT zilizosalimishwa CHADEMA.

“Bado tunachunguza nani aliyezileta ofisini kwetu, leo ni Jumapili tumekutana ili kulifanyia kazi jambo hili, tukio hili ni neema kwa CHADEMA, watu wenye nia njema wanaonyesha wanavyokipenda chama, wameidharau sana ACT, waliopewa na kuzitupa tunawapongeza mno,” alisema Juma.

Kada mwingine wa CHADEMA, Thobias Sebastian, alisema kuwa habari za ndani ambazo chama hicho kimezipata jana, zinadai kuwa kadi hizo, bendera na vipeperushi zilitolewa kwenye ofisi za ACT zilizopo Uyole, ndipo waliyopewa wakazitelekeza CHADEMA.

Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Mbeya, John Mwambigija, alipokea kadi, bendera na vipeperushi vya ACT na kuwapongeza wanachama wa chama hicho walioshawishiwa kukisaliti na kuukana usaliti huo.

“Hali hii imetutia moyo sana, ACT wamekwama watafute wanachama wengi kutoka CCM, huko wanaweza kuvuna sio CHADEMA, kwa kuwa huko tunavuna maelfu kila siku, wasihangaike na CHADEMA hawawezi kuibomoa kirahisi,” alisema Mwambigija.
Hii ni mara ya kwanza katika jimbo la Mbeya Mjini linaloongozwa na CHADEMA, kuokota idadi kubwa ya kadi za chama cha siasa cha upinzani zilizotupwa baada ya kutolewa.

Tanzania Daima ilifuatilia Uyole ili kuwafahamu viongozi wa ACT waliyogawa kadi, bendera na vipeperushi kutoka kwenye ofisi zao, lakini hakuwepo kiongozi yeyote, zaidi bendera ikipepea tu.

No comments: