Wanafunzi wa Shule ya Msingi Azimio wakiwa wamekalia madawati ambayo yametolewa kwa shule hiyo na Benki ya NMB.
Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Nyanda za juu kusini, Lecrisia Makiriye, akitoa taarifa ya msaada wanaokabidhi katika hafla iliyofanyika shule ya Msingi Azimio.
Mstahiki wa Jiji la Mbeya, Atanus Kapunga, akipokea Msaada wa madawati kutoka kwa Meneja wa Nmb kanda kwa niaba ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Meneja wa Nmb Kanda akiwakabidhi wanafunzi wa Shule ya Msingi Azimio Madawati.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kutwa ya Mbeya wakiwa wamekalia baadhi ya madawati yaliyotolewa na Benki ya NMB.
Mkuu wa Shule ya Mbeya, Magreth Haule akipokea msaada wa madawati kutoka kwa Meneja wa NMB Kanda ya Mbeya.
Meneja wa Nmb Kanda pamoja na baadhi ya Walimu wa Mbeya Sekondari wakiwa wamekalia moja ya madawati.
Afisa Uhusiano wa Benki ya NMB, Focus Luhende, akikabidhi madawati kwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mbata.
Walimu
na Wajumbe ya Bodi ya Shule ya Msingi Mbata wakiwa katika picha ya
pamoja na maafisa wa Benki ya NMB mara baada ya kukabidhiwa msaada wa
madawati.
BENKI ya NMB Kanda ya Nyanda za
juu kusini imetoa msaada wa Madawati 214 yenye thamani ya shilingi milioni 15 kwa
Shule tatu zikiwemo Shule za Msingi Mbili na Sekondari moja.
Msaada huo ulikabidhiwa na Uongozi wa Benki ya Nmb katika hafla
iliyofanyika Shule ya Msingi Azimio iliyopo jijini hapa na kupokelewa na
Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, Atanus Kapunga kwa niaba ya Halmashauri ya Jiji
la Mbeya.
Shule zilizonufaika na msaada
huo ni pamoja na Shule ya Sekondari Mbeya iliyopata madawati 84, Shule ya
Msingi Mbata na Shule ya Msingi Azimio
ambazo zimepata madawati 65 kila moja
hivyo kupunguza kwa kiwango Fulani upungufu wa Madawati katika Shule
hizo na kufanya jumla ya madawati 214 yenye thamani ya shilingi Milioni 15.
Akizungumza kabla ya kukabidhi
Msaada huo, Meneja wa Benki ya Nmb Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Lecrisia
Makiriye, alisema Benki yake imelazimika kutoa mchango wa Madawati katika shule
hizo baada ya kupokea maombi pamoja na kutambua changamoto zinazoikabili sekta
ya elimu jambo ambalo wameona lipewe kipaumbele.
Alisema Benki hiyo isingeweza
kupuuzia maombi ya Madawati baada ya kutambua kuwa Elimu ni uti wa mgongo wa
Taifa lolote duniani hivyo kuna umuhimu wa kuwekeza kwenye elimu ili kuwa na
wafanyakazi mahiri na makini pamoja nawananchi walioelimika ambao baadaye
watakuwa wateja wa Nmb.
Awali akimkaribisha Mgeni
rasmi, Afisa Elimu Shule za msingi Jiji la Mbeya,Auleria Lwenza, alisema miezi
sita iliyopita Halmashauri ya Jiji la Mbeya ilikuwa inaupungufu wa madawati
6765 hivyo Msaada wa Nmb utakuwa umepunguza kwa kiwango kikubwa cha Madawati na
kubakia na upungufu wa Madawati 4785 baada ya kupata msaada.
Kwa upande wake Meya wa Jiji la
Mbeya, Atanus Kapunga, mbali na kipongeza Benki ya Nmb kwa msaada wa madawati
katika Shule hizo tatu pia alitoa wito kwa makampuni na taasisi zingine
zinazofanya kazi na uwekezaji katika Mkoa wa Mbeya kuiga mfano wa Nmb kwa
kusaidia kumalizia tatizo la upungufu wa madawati.
Alisema Serikali peke yake
haitaweza kumaliza kabisa tatizo hilo kutokana na kuwa na vipaumbele vingi
jambo ambalo wanaziomba sekta binafsi mashirika, makampuni na wadau mbali mbali
kusaidia changamoto ya madawati kwa Mkoa wa Mbeya ikizingatiwa kuwa ni Mkoa wa
tatu kwa kuliingizia pato taifa.
Nao Walimu wakuu wa Shule
walizokabidhiwa Msaada wa Madawati waliishukuru Benki ya Nmb kwa kukubali
maombi yao ya kuwapatia kiasi cha madawati kutokana na upungufu uliokuwepo na
kwamba itarahisisha ufundishaji na wanafunzi watazingatia masomo.
Mwalimu Magreth Haule, Mkuu wa
Shule ya Sekondari yaKutwa ya Mbeya alisema shule yake kwa mwaka huu ilikuwa
ikikabiliwa na upungufu wa madawati 381 jambo ambalo lilikuwa likisababisha
wanafunzi watatu kukaa dawati moja hivyo kuongezeka kwa utoro, ufaulu kupungua
kutokana na ukaaji kuwakatisha tama wanafunzi.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi
Mbata,Angelina Mwandika,alisema shule
yake ilikuwa na upungufu wa madawati 140 hivyo baada ya kupata msaada huo
itakuwa na upungufu wa madawati 75.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya
Msingi Azimio alisema baada ya kupata msaada kutoka Benki ya Nmb itakuwa na
upungufu wa madawati 79 ambapo alitoa wito kwa wazazi na walezi kusaidia
kumaliza kabisa tatizo hilo.
Na Mbeya.
No comments:
Post a Comment