Tuesday, 22 March 2016

Rais Dkt. Magufuli Atuma Salamu Za Rambirambi Kufuatia Kifo Cha Ghafla Cha Mkuu Wa Wilaya Ya Njombe


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Njombe Dkt. Rehema Nchimbi, kufuatia kifo cha ghafla cha Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Sara Dumba, Kilichotokea jana jioni tarehe 21 Machi, 2016.

Bi. Sara Dumba aliugua ghafla kuanzia jana mchana na baadaye kukimbizwa katika hospitali ya Mkoa wa Njombe (Kibena), ambako wakati akipatiwa matibabu alifariki dunia majira ya saa moja za jioni.

Katika salamu hizo Rais Magufuli ameelezea kushitushwa na kifo cha ghafla cha Bi. Sara Dumba, ambaye amesema alimfahamu kwa uchapakazi wake, uaminifu na uadilifu katika utumishi wa umma na katika uongozi.

"Nimeshitushwa sana na kifo cha Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Sara Dumba, kwa mara nyingine Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye mchango wake ulikuwa bado unahitajika" amesema Rais Magufuli.

Dkt. Magufuli amebainisha kuwa Marehemu Sara dumba atakumbukwa kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuhimiza maendeleo ya wananchi, hususani katika kilimo na ufugaji, kuhimiza nidhamu ya utumishi serikalini na kuwatetea wananchi wa hali ya chini wakati wote wa majukumu yake ya ukuu wa wilaya.

Rais Magufuli amesema anaungana na familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu mkubwa, katika kipindi hiki kigumu na pia amewataka wote kuwa na subira na uvumilivu.

Amemuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina.

Gerson Msigwa

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU

Dar es salaam

22 Machi, 2016

No comments: