Monday, 9 October 2017

Tumbusi hatarini kupotea katika hifadhi za Ruaha na Katavi ikiwa juhudi za makusudi za kiuhifadhi hazitachukuliwa


Tumbusi ndege wala mizoga wapo kwenye hatari kubwa kutoweka kwa vile idadi yao kubwa wamekuwa wakiuawa kwa sumu na baadhi ya wanavijiji kwa mujibu tafiti zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika Afrika mashariki na Afrika kwa ujumla anaripoti  mwanahabari  wetu  Friday Simbaya, Iringa
Kwa mujibu mratibu msaidizi masuala ya ikolojia kutoka shirika lisilo la kiserikali linalo husika na uhifadhi wa wanayampori (WCS) Iringa Msafiri Mgumba alisema hayo jana katika Siku ya Kimataifa ya Uelimishaji jamii  kuhusu Tumbusi, Utafiti unaoendelea kufanyika kwenye eneo la kiikolojia la Ruaha-Katavi unaonesha kuwa changamoto hiyo ipo pia na hifadhi za Taifa za Ruaha na Katavi na Mapori ya Akiba yanayozunguka hifadhi hizo ni eneo muhimu la kiikolojia kwenye uhifadhi wa ndege aina ya Tumbusi..
Hii ni kulingana na utafiti wanaofanya kwa kushirikiana na wataalam kutoka North Carolina Zoo ya Marekani, Hifadhi za Taifa za Tanzania (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).
Hata hivyo, Tanzania inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Uelimishaji wa tumbusi kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi na yaliofanyika katika Kijiji cha Tungamalenga karibu na hifadhi ya Ruaha katika wilaya ya Iringa, mkoa wa Iringa.
Alisema kupitia mpango wa mazingira ya Ruaha-katavi ni muhimu sana katika uhifadhi wa aina 5 za tumbusi ambazo ziko kwenye  hatari kubwa ya kutoweka ikiwa juhudi za kiuhifadhi hazitafanyika ikiwa na pamoja na kutoa elimu. Aina hizo za Tumbusi ni kama vile Kichwa Cheupe, Ruppell’s, Mgongo Mweupe, Kichwa Kikubwa na Kapu chini. Aina mbili zipo kwenye hatari ya kupotea lakini siyo hatari kubwa mathalani Tumbusi kichwa kikubwa
Msafiri alisema kuwa katika tafiti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa sumu ni tishio kubwa kwa idadi ya ndege wala mizoga hasa katika kwenye maeneo ya uhifadhi wa kijamii/Asasi kama vile Matumizi Bora ya Malihai Tarafa za Idodi na Pawaga (MBOMIPA) na maeneo ya vijiji kuzunguka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (RUNAPA).
Alisema kutokana na uchungaji mifugo mbovu ulipelekea ng’ombe alisahaulika machungani na kupelekea simba kuua, kula na kubakiza. Baadhi ya wafugaji wasiotambua umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori waliweka sumu kwenye mabaki ya mzoga wa ng'ombe alieuwawa na ili kumuuwa simba huyo lakini kwa bahati mbaya kundi la tumbusi walienda kula mzoga huo  nakufa, hii ni kutokana kuwa tumbusi anauwezo wa kuona mbali akiwa angani hadi mita 1000 kwa mujibu wa utafiti uliofanyika
Kwa mujibu wa WCS, tumbusi 56 na tai wa kijivu mmoja na ndege wengine aina ya pungu 3 na wanyamapori wengine wanaonyonyesha wawili waliuawa mwezi Mei 2016 kutokana na sumu kwenye eneo la jumuia la MBOMIPA karibu na kijiji cha Tungamalenga kutokana na matumizi mabaya ya sumu kwa baadhi ya wanakijiji wa Tungamalenga katika wilaya ya Iringa, mkoa wa Iringa.
WCS, TANAPA na TAWA wameanzisha kampeni kabambe ya kuelimisha jamii zinazozunguka maeneo ya Uhifadhi kuhusu  ndege hao aina ya tumbusi wanaotegemea mizoga kwa kiasi kikubwa kwa sababu baadhi ya wanavijiji hawajui umuhimu wa ndege na sheria za uhifadhi. Kampeni hii  inajulikana kama ‘SAIDIA KULINDA TUMBUSI’ kwa manufaa ya wanyamapori, utalii, mazingira na uchumi wa jamii yenyewe na taifa kwa ujumla..
Mwaka 2015 hadi sasa, WCS na North Carolina Zoo wamefanikiwa kuwavisha tumbusi 10 vifaa maalum mgongoni, ili kupata taarifa za mtawanyiko wao, wapi wanaenda na wanapata changamoto zipi, na je wanakwenda kwenye hifadhi nyingine au la. Moja ya matokeo ni kuwa ndege wenye vifaa wameweza kwenda Katavi na Mapori ya akiba mengine karibu na za Katavi na Ruaha na kurudi Ruaha. Tumbusi mmoja ameweza Kutoka Ruaha na kuvuka mpaka wa Tanzania na kwenda hadi Afrika ya kusini.  .Tumbusi watatu wa awali waliokuwa wamefungwa vifaa hivyo awali walikufa na inasadikika kuwa ni kutokana na sumu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela aliyekuwa mgeni wa heshima wakati wa Siku ya Kimataifa ya Uelimishaji jamii kuhusu Tumbusi alisema kuwa kuongeza ufahamu kati ya wanakijiji ni mstari wa kwanza wa ulinzi dhidi ya kupungua kwa idadi kutokana na sumu.
Aliwahimiza wanakijiji wasiue ndege hao kwa sababu ni muhimu kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira, wanyamapori, watu, utalii na uchumi. 
Kasesela alisema tumbusi hula wanyama waliokufa kwa haraka na kwa ufanisi.
Alisema kuwa matumbo yao yana tindikali yenye uwezo wa kumeng’enya na kuua kabisa vimelea vya ugonjwa kama kimeta, kufua kikuu na kichaa cha mbwa bila wao kudhurika.
Alisema kuwa uwekaji wa sumu ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa sheria ya uhifadhi wa wanayamapori Tanzania ya mwaka 2009 na sheria ya mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori Tanzania 2013 na kuna adhabu kali kwa yeyote aakayeshikwa akitumia sumu kwa lengo la kuua wanyamapori

No comments: