.
Na Rashid Mkwinda,Mbeya
KUUNGUA kwa Mabweni ya Shule ya Sekondari Iyunga Jijini Mbeya kumeibua kashfa kwa viongozi wa serikali jijini humo wakiwemo Mkuu wa wilaya ya Mbeya Nyerembe Munassa na Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Dkt. Samwel Lazaro wanaodaiwa kuratibu harambee Jijini Dar es salaam na kutapanya zaidi ya milioni 50 kwa maandalizi.
Hata hivyo harambee hiyo iliyopangwa kufanyika Ubungo Plaza March 19 iliahirishwa ghafla huku ikidaiwa kuwa na maandalizi yanayodaiwa kugharimu zaidi ya sh. mil 50 fedha ambazo zingeweza kusaidia ukarabati mkubwa wa majengo ya shule hiyo ambayo ina umri wa miaka 90 tangu ianzishwe.
Kiasi hicho cha fedha ambazo ni sehemu ya maandalizi zimedaiwa kutokana na kukodi ukumbi wa kufanyia harambee hiyo Ubungo Plaza,gharama za kuwasafirisha watendaji wa halmashauri na waandishi wa habari na malazi yao jijini Dar es salaam kwa siku tano pamoja na maandalizi ya Chakula ukumbini.
Gharama za ukumbi na chakula Ubungo Plaza zinakadiriwa kila mtu mmoja anayehudumiwa hotelini hapo ni kiasi cha Sh 77,000 malipo ambayo hufanyika kabla ya kupewa huduma na kuwa kulingana na idadi ya watu 300 walioalikwa kwa ajili ya kushiriki harambee hiyo jumla ya sh. Mil 23.1 zilitumika.
Gharama nyingine zinazoelezwa kutumika kwa maandalizi hayo ni pamoja na posho kwa maafisa wa halmashauri hiyo ambao wanadaiwa kulipwa jumla ya sh mil 9 ikiwa ni takwimu za hesabu za posho na malazi ya Sh120,000 mara siku 5 na waandishi wa habari pamoja na madereva watatu na magari ambapo inadaiwa kila gari moja matengenezo na mafuta kwa safari ya Dar es salaam ni sh milioni 1.
Hali iliyoibua maswali kutoka kwa wadau mbalimbali mkoani Mbeya ni kitendo cha viongozi hao wa serikali kutumia mamilioni ya fedha kwa ajili ya maandalizi ya harambee ya kuchangisha fedha kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza Jijini Dar es salaam badala ya harambee hiyo kufanyika ukumbi wa Mkapa Jijini Mbeya.
‘’Hizi ni mbinu tu za kutafuna fedha za walipa kodi, kutokea kwa janga la moto imekuwa sababu za watu kutafuta mwanya wa kulamba fedha hakuna mantiki ya harambee kwenda kufanyika Dar es salaam badala ya kufanyika hapa Mbeya huu ni ufisadi wa namna yake’’, alisema mkazi wa Iyunga Jijini Mbeya ambaye aliomba ahifadhiwe jina lake kwa kuwa anaishi jirani na shule hiyo.
Mkazi huyo alimuomba Rais John Magufuli kuwawajibisha wote waliohusika kwa namna moja ama nyingine katika sakata hilo kutokana na ukweli kuwa kumekuwa na ubadhirifu wa wazi ulioandaliwa na watendaji wa serikali kutengeneza fursa ya kula mamilioni ya walipa kodi.
Mbunge wa jimbo la Mbeya mjini Joseph Mbilinyi alipoulizwa juu ya sakata hili alikiri kuwa yeye alikuwa ni mmoja wa watu waliohudhuria ukumbi wa Ubungo Plaza kwa ajili ya harambee iliyoandaliwa na viongozi wa serikali ya jiji la Mbeya na kuwa hata hivyo harambee hiyo iliahirishwa katika hali ya utata.
‘’Mimi ni kati ya waalikwa waliohudhuria kwenye harambee hiyo,watu wengi walijitokeza ukumbini Mkuu wa wilaya ya Mbeya alijitokeza ukumbini na kuahirisha harambee hiyo,’’alisema Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu.
‘’Mimi sio msemaji, wasemaji ni waandaaji ambao ni serikali ya Jiji la Mbeya, mimi na wenzangu tulihudhuria kama waalikwa maandalizi yote ya harambee yalifanywa na Viongozi wa Jiji na Mkuu wa wilaya,’’alisema Mbilinyi.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya Maafa Marcel Ipini akizungumzia suala hilo alisema kuwa mara baada ya mabweni ya shule ya sekondari Iyunga kuteketea kwa moto iliundwa kamati ya maafa ambayo yeye ndiye Mwenyekiti na kuwa hata hivyo taarifa za kuwepo kwa harambee Jijini Dar es salaam alizisikia kwenye vyombo vya habari tu.
‘’Mimi kama Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa sikuwa na taarifa za harambee ya Ubungo Plaza, harambee niliyoijua ilikuwa ifanyike Machi 23 ukumbi wa Mkapa, taarifa za harambee za Ubungo Plaza ambayo tulisikia kuwa mgeni rasmi atakuwa Waziri mkuu nimeisikia kupitia vyombo vya habari,’’alisema Ipini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya shule ya sekondari Iyunga Stephen Mwakajumilo alisema kuwa hakuhusishwa na harambee iliyopangwa kufanyika Ubungo Plaza na kuwa bodi ya shule hiyo ilikuwa na mpango wa muda mrefu kwa kuwahusisha wanafunzi wote waliosoma shuleni hapo kusaidia uboreshaji wa miundo mbinu tangu mwaka 2014.
‘’Sisi tulianza mkakati wa maboresho ya miundo mbinu ya shule hiyo tangu mwaka 2014, tulilenga wanafunzi waliowahi kusoma Iyunga popote walipo, lengo letu lilikuwa ni kufanya Fund Rising ilikuwa bado hatujaandaa, lilipotokea janga hili, Mkuu wa wilaya ya Mbeya na Mkurugenzi wa Jiji wakaamua kufanya harambee Jijini Dar es salaam ambayo sisi hatukuhusishwa’’alisema.
Aidha kwa mujibu wa msimamizi wa ufyatuaji tofali za shule hiyo Mchungaji Thomas Kabigi alisema kuwa bweni moja linachukua takribani tofali 6,500 ambapo gharama ya tofali moja inafikia sh.300 na kuwa kutokana na hesabu hiyo ya msimamizi wa ufyatuaji wa matofali bweni moja linaweza kumalizika kwa tofali zenye gharama ya sh milioni 1.95.
Kutokana na hesabu hizo kiasi hicho cha fedha jumla ya sh.mil 50 zinazoelezwa kuwa huenda zilitumika kwa ajili ya maandalizi ya harambee iliyoshindwa kufanyika zingeweza kufyatua matofali mengi zaidi ambayo yangekidhi kufanya ukarabati mkubwa wa shule hiyo kongwe nchini.
Kulingana na taarifa za awali kupitia matangazo yaliyokuwa yakitangazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini ni kuwa jumla ya sh.mil 700 zilikuwa zikihitajika kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya shule hiyo ambazo zingeweza kupatikana kutokana na harambee iliyotakiwa kufanyika Ubungo Plaza.
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Mbeya Charles Mwakalila alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema kuwa maandalizi yote ya harambee hiyo yalikuwa yakifanywa na Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi wa Jiji na kwamba kwa sasa shule hiyo mwajiri wake ni TAMISEMI baada ya kugatuliwa kwa madaraka kutoka serikali kuu.
‘’Kwa sasa shule hiyo iko chini ya Halmashauri ya Jiji kwa kila jambo,maandalizi na mambo yote yanayoihusu shule hiyo yapo chini ya Serikali za Mitaa, mkoa hauhusiki na lolote,’’alisema Mwakalila.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Dkt Samwel Lazaro alipotakiwa kuelezea sakata hilo baada ya kupigiwa simu yake ya kiganjani alikataa kuelezea lolote juu ya suala hilo na kumtaka mwandishi kuwaeleza wengine wanaofuatilia jambo hilo kuwa yeye hana jibu lolote kwa sasa.
‘’Tafadhali naomba msiniulize jambo lolote kuhusiana na harambee, waambie na wenzio wanaofuatilia jambo hilo sina lolote ninaloweza kulizungumzia,’’alijibu Dkt Lazaro na kukata simu yake baada ya kupigiwa simu kutoa ufafanuzi juu ya sakata hilo.
Naye Mkuu wa wilaya ya Mbeya Nyerembe Munassa alipozungumza na gazeti hili alidai kuwa mazingira ya kuahirishwa kwa harambee hiyo yaligubikwa na utata, ‘’harambee iliahirishwa dakika za mwisho lazima tuwe honest tutajipanga vizuri,ukiambiwa uahirishe, unaahirisha,tuliambiwa kulikuwa na uchaguzi Zanzibar viongozi hawawezi kuwepo,’’alisema Munassa.
Taarifa za kiuchunguzi ambazo gazeti hili inazo zinaeleza kuwa kuahirishwa kwa harambee hiyo kumetokana na mambo ya kisiasa kwa baadhi ya wanasiasa kudaiwa kutaka kupatia umaarufu tatizo la Iyunga na hivyo njia pekee bila kujali hasara iliyokuwepo ilikuwa ni kuzuia harambee hiyo isifanyike.
‘’Kufanyika kwa harambee hii kungewapaisha watu kisiasa, unajua sasa hivi watu wako njia panda ukifanya kitendo kimoja tu kizuri kinaweza kukupaisha na ukifanya kitendo kimoja tu kibovu kinaweza kukushusha kwa sakata hili watu watashushwa tu,’’alisema mdau mmoja wa elimu ambaye naye hakupenda kutajwa jina lake kwa madai ya kuwa ana maslahi katika shule ya Iyunga.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makalla ambaye alikuwa akifuatilia mjadala wa sakata hilo kupitia mtandao wa Facebook kutokana na kichwa kilichosema Amos Makala akaribishwa kwa skendo mkoani Mbeya alisema kuwa amefuatilia kwa makini sakata hilo na kuwa kwa sasa yupo nje ya mkoa bali atakuwa na ziara April 5 shuleni hapo.
‘’Nina ziara ya kutembelea maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mbeya hapo Iyunga Sekondari nitatumbua hilo jipu siku hiyo ya tarehe 5,’’alisema Makalla.
Chanzo:Majira
No comments:
Post a Comment