Mbeya. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mbeya Mjini
kimesema safu ya viongozi wa jumuiya za chama hicho zilizofanyika
mwishoni mwa mwezi uliopita zitawasaidia kurudisha jimbo la Mbeya Mjini
na halmashauri mikononi mwake katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Katika
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, CCM Mbeya Mjini ilishindwa kumng’oa mbunge
wa jimbo hilo, Joseph Mbilinyi 'Sugu’ (Chadema) lakini ilijikuta
ikipoteza viti vingi vya udiwani jambo lililofanya Chadema kunyakuwa na
halmashauri ya jiji hilo baada ya Chadema kuwa na viti 26 vya udiwani na
CCM kumi.
Kwa nyakati tofauti viongozi waandamizi wa CCM Mbeya Mjini wamesema mfumo wa uchaguzi ulioanzishwa sasa na chama hicho unaondoa msuguano na makundi yanayojenga fitina, majungu na usaliti tofauti na hapo awali.
Katibu
wa Umoja wa Wazazi-CCM Wilaya ya Mbeya, Sadick Kadulo amesema kwa
sasa CCM ipo makini katika chaguzi zake lengo ni kuona inakuwa na
viongozi wenye uwezo wa kukisaidia chama kukomboa jimbo na halmashauri.
“Mapinduzi
haya ya kimuundo ndani ya chama chetu yana tija sana tofuati na huko
nyuma kwani wakati ule ilikuwa rahisi sana wagombea kucheza rafu ndani
na nje ya chama, na hii ndio iliyotufanya tupoteze jimbo kwa mara ya
pili lakini kubwa zaidi tukapoteza halmashauri,”
“Lakini
naamini hii safu tuliyoipata katika jumuiya zote za CCM ni makini na
imara kutokana na mfumo wake, hivyo katika chaguzi za Serikali za Mitaa
mwaka 2019 tutashinda kwa kishindo lakini pia 2020 tutakomboa jimbo na
halmashauri pia,” amesema Kadulo.
Akiwa wilayani
Mbarali, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya, Dk Mary Mwanjelwa
amewaambia wafuasi wa CCM kwamba chuki, ubinafsi, usaliti na fitina
ndizo zinazokiumiza chama chake Mbeya Mjini na kusababisha kuanguka
katika chaguzi zake tofauti na wilaya nyingine za mkoa huo.
“Mimi
ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoa mzima wa Mbeya, nina wilaya sita, lakini
sijaona mbunge kama mbunge wa Mbarali (Haroon Pirmohamed) na hili
nalizingumza bila kumung’unya maneno, Mbarali tumepata mbunge ambaye ni
lulu tumtumie’.
Hata hivyo amesema jimbo la Mbeya Mjini
ndio kioo cha mkoa mzima wa Mbeya hivyo ni aibu kuona upinzani ndio
unaotawala kuanzia ubunge hadi halmashauri, hivyo anaamini katika safu
za viongozi wapya waliopatikana hawataendekeza makundi ambayo huwa
yanawagharimu siku za uchaguzi, badala yake watakuwa kitu kimoja.
Credit to MWANANCHI
Credit to MWANANCHI
No comments:
Post a Comment