Tuesday 21 June 2016

Serikali Yaagiza Wakimbizi Wanajeshi, Wenye Silaha Wajisalimishe


Serikali ya Tanzania imewataka wakimbizi wote ambao walikuwa wanajeshi kutoka nchi walizokuwepo, kuripoti kwenye mamlaka husika ili waweze kupewa uangalizi maalum (special protection) kama wanajeshi.

Kauli hiyo ya serikali imetolewa na Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali (Mstaafu) Emmanuel Maganga, wakati wa maadhimisho ya siku ya wakimbizi duniani yaliyofanyika kambi ya wakimbizi Nyarugusu, wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.

Alisisitiza kuwa wakimbizi ambao wako nchini wakijua ni wanajeshi ni lazima wasajiliwe na mamlaka husika.

Aidha Maganga aliwataka vile vile wakimbizi wote ambao wanamiliki silaha wazisalimishe kwa hiari yao wenyewe.

Alisema kumekuwa na matukio mengi ya ujambazi wa kutumia silaha na hivyo kuhatarisha amani na kuwaamuru wenye silaha kuzisalimisha mara moja ili waende sawa na sheria za nchi walikopata hifadhi.

 

Mkuu huyo wa mkoa pia alitoa wito kwa mashirika ya misaada duniani kutoa misaada inayoowana na misaada inayotolewa kwa nchi zilizoendelea na kuongeza kuwa mahitaji ya binadamu ya msingi hayatofautiani iwe nchi zilizoendelea au zinazoendelea.

Alisema kuwa wakimbizi waliopo kwenye nchi zilizoendelea hupewa makazi ya kudumu na vyakula tofauti tofauti wakati waliopo kwenye nchi zinazoendelea hupewa mahema na chakula aina moja ambayo ni mahindi.

“Mwaka jana tulishindwa kuadhimisha siku ya wakimbizi duniani kwa kuwa tulikuwa tunawapokea wakimbizi kutoka Burundi,” alisema.

Alisema wakimbizi wameongezeka sana nchini na sasa hivi kuna makambi matatu yanayowahifadhi wakimbizi nchini.

 

Wakati huo huo Tanzania imepongezwa kwa ukarimu wake kwa kuwahifadhi wakimbizi kwa zaidi ya miongo minne sio tu kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na hata duniani.

Mwakilishi mkazi wa shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR , Chansa Kapaya alisema hayo katika sherehe za kuadhimisha siku ya wakimbizi duniani yenye kauli mbiu kuwa “Tupo Pamoja na Wakimbizi, Tafadhali ungana nasi”.

“Tanzania ni mfano wa kuigwa kwa mfano mzuri wa kuwahifadhi wakimbizi wengi duniani na pia kuwatafutia suluhu,” alisema.

Alisema mwaka 2014 Tanzania iliwapa uraia wakimbizi zaidia ya 162,000 baada ya kuishi nchini kwa zaidi ya miaka 40.

Aliongeza kuwa, wakimbizi wanapaswa kuthaminiwa kama binadamu wengine kwa kuwa hakuna mtu anayechagua kuwa mkimbizi.

Kapaya alisema kuwa kwa sasa kambi ya Nyarugusu ina wakimbizi zaidi ya 131,733 ambao ni wengi zaidi na kusababisha msongamano unaohatarisha maisha yao.

No comments: