Monday 20 June 2016

Serikali Yasitisha Ajira Zote Kwa Muda


SERIKALI imesitisha ajira zote, kama njia ya kukabiliana na wimbi la watumishi hewa.

Kutokana na uamuzi huo hivi sasa hakuna nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa Serikali na wakala zake pamoja na utoaji wa vibali wa likizo ya bila malipo.

Katibu Mkuu Utumishi, Dk. Laurean Ndumbaro,  jana alisema kuwa Serikali imesitisha kwa muda utoaji wa ajira, ili kupitia upya muundo wa Serikali na taasisi zake.

Alisema utekelezaji wa mkakati huo utakwenda sambamba na kusitisha kwa muda utoaji wa vibali vya ajira zote mbadala pamoja na uidhinishaji wa ajira hizo zilizopo Sekreterieti ya Ajira katika utumishi wa umma na kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi.

“Ni kweli tumesitisha kwa muda ili kupitia mfumo wa Serikali na hata kuangalia ulipaji wa mishahara kama upo katika malipo stahiki.

“…na hili litakwenda sambamba na hata kusitishwa malipo ya mishahara yanayotokana na upandishwaji wa vyeo kwa watumishi. Tukimaliza zoezi hili ndipo tunaweza kuanza kutoa ajira za Serikali,” alisema Dk. Ndumbaro.

Alisema muundo mpya wa utumishi wa Serikali unakwenda sambamba na uhakiki wa malipo ya mishahara, hivyo ni lazima ujue ni nani unayemlipa kuliko ilivyo sasa.

Kwa mujibu wa maelekezo hayo uhamisho na uidhinishaji katika mfumo wa watumishi ambao wamehamishwa kutoka kwa mwajiri mmoja kwenda kwa mwajiri mwingine ambao atalipwa mshahara mkubwa kuliko ule wa sasa pia utaangaliwa kwa lengo la kupata taarifa sahihi za mtumishi husika.

“Baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki watumishi pamoja na tathmini ya muundo wa Serikali na taasisi zake, wote wataarifiwa ni lini utekelezaji utaendelea,”alisema.

Taarifa kutoka maeneo mbalimbali nchini, zinaarifu kuwa maelekezo hayo yalitolewa Juni 13, mwaka huu na kusambazwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwa makatibu wakuu wote, makatibu tawala wa mikoa, kwa wakuu wa idara za Serikali zinazojitegemea.

Waliotakiwa kutekeleza maelekeo hayo ya Serikali ni wakurugenzi wote wa majiji, manispaa na miji, wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya, watendaji wa taasisi za umma na watendaji wa wakala za Serikali kwa upande wa Tanzania Bara.

Kamatakamata

Wiki iliyopita vyombo vya dola vilianza kuwatia mbaroni watumishi hewa kwa kuwafuata na pingu majumbani.

Hatua hiyo imetajwa kuwa ni mkakati wa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, kuanza kupambana na watendaji ambao wamekuwa wakiisababishia hasara Serikali ya kulipa mamilioni ya shilingi kwa watumishi hewa.

Kutokana na uamuzi huo  ambapo mtumishi mmoja wa moja  za Mkoa wa Kigoma, alifuatwa na askari wa polisi na kutiwa mbaroni nyumbani kwao Ubungo Kibangu jijini Dar e Salaam.

Tukio hilo la aina yake lilitokea mchana wa juzi na kuibua hisia miongoni mwa majirani ambao waalisema kuwa, askari hao walifika nyumbani kwao na mtumishi huyo na kumfunga pingu mikono na miguuni na kuondoka naye.

Kutokana na hekaheka hiyo ya watumishi hewa, taarifa kutoka wilayani Nyasa mkoani Ruvuma, zilidai kuwa walimu watano wastaafu nao walikamatwa na polisi kwa madai ya kupokea mishara hewa.Mbali na walimu hao pia alikuwepo muuguzi mmoja.

Hivi karibuni akizungumza Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, alisema Serikali imewaondoa jumla ya watumishi 12,246 kwenye mfumo wa malipo ya mishahara kwa sababu mbalimbali, ikiwemo umri wa kustaafu kwa lazima, kufukuzwa kazi, vifo na kumalizika kwa mikataba.

Waziri Kairuki alisema kuondolewa kwa watumishi hao kumeokoa Sh bilioni 25 ambazo zingelipwa kwa watumishi hao.

Alisema kuwa fedha hizo zingepotea endapo watumishi wasingeondolewa kwenye mfumo, ikilinganishwa na watumishi 10, 295 walioondolewa kwenye mfumo kuanzia Machi 15 hadi Aprili 30 mwaka huu.

Alisema pia kuwa watumishi hewa 1,951 wameongezeka ikiwa ni pamoja na Sh bilioni 1.8.

Alifafanua kuwa ofisi hiyo ilitoa maelekezo kwa Makatibu Wakuu, Wakuu wa taasisi za umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuwasilisha taarifa ya watumishi hewa ifikapo Juni 10, mwaka huu. 

Chanzo: Mtanzania

No comments: