Thursday 25 August 2016

Mahabusu Ajinyonga Arusha


Mahabusu aliyekuwa akishikiliwa katika kituo kikuu cha polisi jijini Arusha aliyetambulika kwa jina la Victoria Wenga (51) mkazi wa Lemara jijini Arusha amejinyonga hadi kufa usiku wa kuamkia jana kwa kutumia shuka lake bila kuacha ujumbe wowote.

Marehemu alikamatwa Agosti 21 mwaka huu majira ya Alfajiri kwa tuhuma za kuchoma moto nyumba yake na maduka yake mawili kutokana na ugomvi wa kifamilia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alikiri kutokea kwa tukio hilo katika Kituo cha Kikuu cha Polisi saa 6:20 usiku jana wakati wenzake wakiwa wamelala.

“Polisi wa zamu alisikia kelele kutoka kwenye chumba cha mahabusu wa kike ambapo polisi walijitahidi kuokoa maisha ya mahabusu huyo, lakini ilishindikanika,” alisema Kamanda Mkumbo.

Mahabusu huyo, ambaye ni mkazi wa Lemara jijini Arusha, alijinyonga kwa kutumia shuka lake alilokuwa anatumia kujifunikia wakati yuko mahabusi. Mtuhumiwa huyo, alijinyonga kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka yake.

“Jana ilikuwa afikishwe mahakamani kujibu kosa lililokuwa linamkabili,”alisema Kamanda Mkumbo na kuwahakikishia kuwa hali ya usalama kituoni hapo na tukio hilo, havihusiani na sababu zozote za kiusalama.

Marehemu Victoria anadaiwa kuwa na ugomvi wa kifamilia na mume wake aliyetambulika kwa jina la Edward Wenga akimtuhumu kuzaa nje ya ndoa kinyume na utaratibu.

Imeelezwa kuwa  hicho ndo chanzo cha marehemu kufikia hatua ya kuteketeza mali walizochuma na mume wake ambazo ni maduka mawili na nyumba ya kuishi.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuifadhia mahiti Hospitali ya Mount Meru.

No comments: