USAFIRI wa treni ndani ya Jiji la Dar es salaam umeanza
rasmi leo na kupokelewa kwa furaha .
Treni hiyo inatarajiwa
kuwa mkombozi wa tatizo la usafiri
katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam.
Kuanza kwa usafiri huo, ni utekelezaji wa ahadi ya Waziri wa
Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, katika kikao cha Bunge cha bajeti ambapo
alisema usafiri huo ungeanza Oktoba mwaka huu na hivyo kupungua adha ya usafiri
kwa wananchi wa Jiji la Dar es salaam.
Uzinduzi wa safari hiyo uliofanywa kwa njia mbili, ya kwanza kuanzia
Ubungo hadi Stesheni chini ya Kampuni ya
Reli Tanzania (TRL) na nyingine kuanzia Mwakanga hadi Kurasini.
Treni hiyo iliyokuwa na mabehewa sita likiwemo moja
lililotengwa maalumu kwa ajili ya wanafunzi, ilionekana kufurahiwa na wananchi waliokuwa wamepanda kutokana na utulivu
uliokuwamo ndani yake huku ukisindikizwa
na burudani za muziki na matangazo kutoka kwa wahudumu waliokuwemo ndani ya
kila behewa.
Akizungumza mara baada ya kuzindua usafiri wa treni itokayo
Ubungo hadi Stesheni, Waziri Mwakyembe
aliwataka wafanyakazi wa Shirika hilo kuweka pembeni kero zao na
kuongeza nguvu katika maboresho ya usafiri huo kwa lengo la kuliletea tija
Taifa.
Alisema ujio wa usafiri huo ni maendeleo makubwa kwa uchumi wa
Jiji la Dar es salaam na Taifa kwa ujumla kwa kuwa utaongeza ufanisi katika
utoaji huduma za usafiri .
Nauli ya usafiri huo ni Sh 400 kwa kila mtu mzima na Sh 100
kwa mtoto au mwanafunzi kwa treni ya Ubungo hadi Stesheni huku treni ya Tazara
ikitoza Sh 500 kwa mtu mzima na Sh 100 kwa mtoto au mwanafunzi.
No comments:
Post a Comment