Tuesday, 30 October 2012

MGANGA WA JADI AUAWA BAADA YA WATEJA WAKE KUTOPATA MATOKEO MAZURI YA MATATIZO YAO.


 
*Wamlipa Mganga shilingi 600,000/=
*Waacha ujumbe wanakijiji wasihusishwe.
 
Watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamemuua kwa kumkatakata na mapanga kisha kumpiga nyundo utosini Mganga wa Jadi, aliyetambuliwa kwa jina l.a Mlenga Mwazowa(60 - 65, mkazi wa Kitongoji cha Izumbwe, Kijiji cha Inyala Wilaya ya Mbeya Vijijini Mkoani Mbeya.

Tukio hilo limetokea Oktoba 27 mwaka huu majira ya saa sita usiku, ambapo watu hao walivunja nyumba ya mganga huyo kisha kumtoa nje na kuanza kumchalanga kwa mapanga na kisha kumpiga nyundo ya utosini, ambapo alifariki papo hapo mita chache kutoka kwenye nyumba yake.

Imedaiwa kuwa mganga huyo alikuwa na ahadi na wateja wake ambao walilipa kiasi cha shilingi 600,000 kwa minajili ya kutimiziwa malengo yao lakini baada ya kulipa kiasi hicho na kutofikiwa wanaji hao walimfuata na kumtaka arudishe pesa hizo lakini Mganga huyo alishindwa ndipo walipotekeleza azma yao kisha kuacha ujumbe kwenye karatasi ulioandikwa "ASIKAMATWE MTU YEYOTE KATIKA TUKIO HILI KWANI MGANGA AMEKULA LAKI SITA ZETU NA HAJATEKELEZA AHADI YETU" ulimaliza ujumbe huo na kwamba tumetoka Ngolongo.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bwana Herman Mwanyinaga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba aliamshwa majira ya saa saba usiku na alifika eneo la tukio na kwamba wakati ukatili huo unafanyika mke wa marehemu alikuwa ndani na wanawe watatu.

Mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu zake baada ya kufanyiwa uchunguzi na Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya cha Inyula kilichopo wilayani humo.

Hata hivyo hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hili na mazishi yalifanyika nyumbani kwa marehemu Oktoba 27 majira ya saa saba mchana. 

No comments: