Sunday, 3 November 2013

M23 WAANZA MAPAMBANO UPYA

m23 3202f
*Mazungumzo ya Uganda yakwama tena, Bisiimwa asema yeye si mtu rahisi
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni
KIKUNDI cha waasi wa M23, jana asubuhi kimeanzisha upya mapigano dhidi ya Jeshi la Serikali ya Kongo (FARDC), linaloshirikiana na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa (MONUSCO), katika eneo la Mashariki mwa mji wa Goma, RAI Jumapili limedokezwa. (HM)

Mashambulizi hayo ya waasi wa M23 yamekuja saa chache baada ya kuvunjika kwa mazungumzo ya amani usiku wa kuamkia jana, yaliyokuwa yakifanyika mjini Kampala, Uganda, chini ya Mwenyekiti wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), Rais Yoweri Museveni.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana kutoka kwa chanzo chake kinachoaminika, kilichoko uwanja wa mapambano nchini Kongo, zilieleza kuwa waasi hao wameanzisha mashambulizi ya kurejesha himaya zao zilizopo katika mji wa Rumangabo, ambazo walipokonywa hivi karibuni na Jeshi la Congo (FARDC).
"Kwa sasa nipo kwenye eneo la Milima ya Kinyori, ambayo inapatikana karibu na mpaka wa Rwanda na Uganda, huku mashambulizi ni makali, ninachokiona hapa ni helikopta ya kivita ya M23 ikijiandaa kuruka kwa ajili ya kushambulia maeneo yanayoshikiliwa na wanajeshi wa FARDC," kilisema chanzo chetu hicho.
Wakati hayo yakijiri, zipo taarifa zinazoeleza kuwa ndege ya kijeshi ya Serikali ya Kongo juzi ilianguka na kulipuka moto, wakati ikijaribu kutua katika Uwanja wa Ndege wa Bangoka, uliopo mkoani Ituri.
Kwa mujibu wa habari zilizolifikia gazeti hili, ndege hiyo ilikuwa imebeba silaha za kivita, lakini bado haijajulikana mara moja chanzo cha ajali yake.
Wakati huo huo, habari ambazo gazeti hili limezinasa kutoka nchini Uganda kulikokuwa kukifanyika mazungumzo ya kuleta amani nchini Kongo, zinaeleza kuwa kwa mara nyingine waasi wa M23 na Serikali ya Kongo wameshindwa kuafikiana na hivyo mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea yamevunjika usiku wa kuamkia jana.
Inaelezwa kuwa kuna mambo matatu ambayo yamesababisha kuvunjika kwa mazungumzo hayo.
Mambo hayo ni pamoja na Serikali ya Kongo kutakiwa kukubali kutoa msamaha kwa makamanda wa waasi wa M23, jambo ambalo lilikataliwa na upande wa serikali, kwa madai kuwa makamanda hao wanashutumiwa na Umoja wa Mataifa kwa makosa ya jinai, ikiwamo kuwatumikisha watoto kijeshi, kutekeleza mauaji pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Sharti la pili ambalo lilisababisha mvutano na hivyo kushindwa kufikia muafaka ni lile la kuitaka Serikali ya Kongo iwajumuishe wapiganaji wa M23 katika Jeshi la Serikali (FARDC), ambapo kwa upande wa serikali ulishauri kwamba wapiganaji wa M23 washushe silaha zao chini, halafu wajikusanye katika kambi moja ya kijeshi, jambo ambalo lilipingwa vikali na viongozi wa M23.
Kwa upande wa sharti la tatu, waasi wa M23 walitaka viongozi wao wajumuishwe katika Serikali ya Kongo, hata hivyo Serikali ya Kongo imegoma kwa madai kwamba viongozi wa serikali ya nchi hiyo hutokana na demokrasia ya kupigiwa kura na wananchi, hivyo wakahoji M23 watakuwa wamepigiwa kura na nani?
Kabla ya kuvunjika kwa mkutano huo, RAI Jumapili ilifanya mahojiano kwa njia ya simu toka nchini Uganda na Rais wa M23, Bertrand Bisiimwa, ili atoe ufafanuzi wa taarifa tata zilizomhusisha na kujisalimisha kwa jeshi la Uganda (UPDF).
Kiongozi huyo alikanusha taarifa hizo na kusema kuwa yeye hawezi kamwe kujisalimisha na kwamba si mtu rahisi kukamatwa.
Akizungumzia wapiganaji wake kuchakazwa vikali na jeshi la Serikali ya Kongo, likishirikiana na kikosi maalumu kinachoundwa na Umoja wa Mataifa cha Force Intervention Brigade (FIB) usiku wa kuamkia Jumatano wiki hii na kusababisha kukimbia ngome yao ya Rumangabo, Bisiimwa alisema hawakukimbia mapigano, ila walirudi nyuma kwenye uwanja wa mapigano ili kutoa nafasi ya mazungumzo ya amani yanayofanyika mjini Kampala.
"Nipo kwenye mkutano mjini Kampala, kwa hiyo sina muda wa kuongea kwa kirefu, sisi hatujakimbia, ila tumetoka katika mstari wa mbele wa mapambano ili kupisha mazungumzo haya...nashangaa habari zilizoenezwa kwamba nimejisalimisha kwa jeshi la Uganda, kwa nini nifanye hivo, mimi si mtu wa kukamatwa kirahisi," alisema Bisiimwa.
Katika hatua nyingine, kiongozi huyo wa M23 alikanusa habari za kumeguka kwa kundi lake na kuunda kikundi kipya cha waasi kilichoanzishwa hivi karibuni, kinachojulikana kwa jina la M18.
Bisiimwa alisema kikundi hicho anakisikia tu, kwamba kipo katika Mkoa wa Ituri, ambao upo Kivu Kaskazini, eneo ambalo lipo mbali sana na sehemu ambayo vikosi vya M23 vinatawala.
Waasi wa M23 walikuwa wamejizatiti katika kambi zao tatu zilizopo katika mji wa Rumangabo, ambao unapatikana kilomita 50 kutoka mji wa Goma, baada ya kuzidiwa nguvu na kufurumushwa katika mji wa Goma na FIB kwa kushirikiana na Jeshi la Serikali ya Kongo Agosti, mwaka huu.
Baada ya mashambulizi makali yaliyofanywa na Jeshi la Serikali ya Kongo Jumatano ya wiki hii, waasi hao waliukimbia mji wa Rumangabo na kutokomea katika milima ya Mbuzi, Chanzori, Kinyori na Chanzi. Chanzo: mtanzania

No comments: