Tuesday, 7 October 2014

Wananchi waaswa kutumia viongozi kuwaletea maendeleo si kuwaomba fedha


Na, Israel Mwaisaka, Nkasi
MWENYEKITI wa umoja wa wanawake mkoa wa Rukwa (UWT) kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Omelina Mgawe amewataka wananchi kuwatumia vyema viongozi wao hususani wabunge na Madiwani katika kusukuma maendeleo na si vinginevyo.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ntatumbila, mkoani hapa, mwenyekiti huyo amesema, kazi kubwa ya Wabunge na Madiwani ni kuihamasisha serikali kutatua changamoto mbalimbali katika maeneo wanayoyaongoza lakini jamii imekua ikiwatumia vibaya viongozi hao kwa kutaka kuwapatia fedha.
Amesema viongozi hao hawakuchaguliwa ili waweze kutoa fedha zao za mifukoni bali kuwawakilisha wananchi serikalini juu ya changamoto mbalimbali zinazojitokeza na kuwa viongozi hao si kazi yao kutoa fedha kwa watu na kuwa fedha hizo hata wao hawana.
Hivyo amewataka wananchi kuendelea kuwatumia vyema viongozi hao katika kusukuma maendeleo yao na kuendelea kuilinda amani iliyopo sasa iliyoasisiwa na Chama cha Mapinduzi na kamwe wasidanganyike na baadhi ya watu ambao lengo lao kubwa ni kuharibu amani ya nchi iliyopo sasa.
Pia Mwenyekiti huyo, ametembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikai katika kijiji hicho ambapo amejionea zahanati na nyumba za watumishi wa zahanati hiyo na kutoa mchango kusaidia ujenzi wa nyumba hizo

No comments: