Saturday, 20 June 2015

Urais 2015: Mwakyembe Achukua fomu, Azungumzia Sakata la Richmond


Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe, amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa na CCM kugombea urais, huku akisema hana chuki na mtu yeyote kwa sababu sakata la Richmond halikuwa la kwake bali ni la Bunge.

Akizungumza jana mjini Dodoma, Dk Mwakyembe alisema ameamua kuomba kuteuliwa kwenye nafasi ya urais kwa sababu anataka kupeperusha bendera ya CCM katika kinyang’anyiro hicho, akitekeleza haki yake ya kikatiba na kidemokrasia.

Pia alisema kitendo chake cha kujitokeza kuwania urais, kinatoa fursa pana kwa CCM katika kuchambua majina ya wagombea ili kumpata mtu sahihi zaidi.

“Mimi ni sehemu ya Serikali ya awamu ya nne, kwa hiyo nina uelewa wa kina wa changamoto ambazo zimewakabili katika kusukuma maendeleo yetu. Lakini vile vile ni shahidi wa mafanikio mengi sana ya Serikali ya awamu ya nne chini ya CCM,” alisema Dk Mwakyembe.

Aliongeza, “Nazitambua fursa tele za kuweza kusukuma nchi yetu mbele, tofauti na miaka mingine yote mimi ndani ya sakafu ya moyo wangu natambua kabisa tutaingia katika uchaguzi wa mwaka 2015 tukiwa na mifano halisia ya ufanisi, kwa hiyo hatuingii tukiwa tumenyong’onyea, tumejikunyata, hapana kwa sababu tumefanya mengi mazuri na mengi mazuri yanakuja chini ya serikali ya awamu ya tano.”

Alipoulizwa kuhusu vipaumbele yake, Dk Mwakyembe alisema yeye si mgombea binafsi bali anatokana na CCM.

“Kwa sababu sisi tuna uzoefu wa kuiongoza hii nchi, si akili ya mtu mmoja kusukuma gurudumu la maendeleo tunaweka vichwa pamoja tunatoka na kitu kinachoitwa Ilani ya uchaguzi ya miaka mitano.

"Na mimi nakuhakikishia ikitoka na kukabidhiwa nitaitafsiri mimi na kutumia ubunifu, kujituma, uzalendo na mapenzi kwa nchi yangu nitaitekeleza kwa dhati,”alisema.

Dk Mwakyembe alisema chini ya awamu ya nne wamefanya mambo mengi na yeye ataendeleza na kwamba kila awamu inayokuja inafanya vizuri zaidi.

Azungumzia Richmond
Kuhusu Kamati ya kuchunguza Richmond iliyomfanya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu, alisema kuwa kazi ile ilifanywa na Kamati ya Bunge na ripoti ilikuwa ni ya Bunge.

“Nilitimiza wajibu wangu kwa roho safi kwa kumtanguliza Mungu, Naapa mbele ya Mungu naamini anatusikia mimi ni muumini mkubwa wa Mungu na ndiye anatufanya tuwe hai, sina chuki na mtu yeyote kwa sababu suala hilo halikuwa langu lilikuwa la Bunge,”alisema na kuongeza:

"Kila nikisikia hivyo inanishtua sana mpaka ninaomba kwa Mungu anisaidie, kama kuna mtu yeyote anakitu chochote moyoni kwa sababu mimi sina,”.

Alisema kuwa watu waliohusika kutuma ujumbe mfupi wa maneno kuwa yeye ameapa kufa au kupona kuhakikisha Lowassa haingii madarakani, wameshakamatwa.

“Na mimi naapa kuwa ni lazima niwafikishe mahakamani waliohusika kusambaza ujumbe huo. Kibaya cha yote mmoja wa vijana hao (waliokamatwa), ni mpambe wa wanaogombea urais. Sisi tunaomba uteuzi wa chama kama watoto wa baba mmoja mama mmoja,”alisema na kuongeza;

“Kuna kitu gani hapa cha uhasama leo nikiteuliwa nategemea kuwa wote hawa wanipongeze, na mimi atakayeteuliwa mwingine mimi nitakuwa namba moja kumpigia debe kwa sababu mimi ni CCM yule ni ndugu yangu.”

Alisema alishtushwa zaidi baada ya mmoja wa vijana waliokamatwa katika tuhuma hizo, kukiri kuwa pia wamepewa kazi ya kuikarabati ripoti ya Richmond halafu wasambaze. Alisema alimweleza kijana huyo akifanya hivyo atafungwa.

“Naapa mbele za Mungu, sina chuki na mtu, kwa sababu suala halikuwa langu, aliyehusika ni kaka yangu namheshimu sana, lakini ninapopewa wajibu wa kufanya sina kaka, sina dada, sina ndugu kama umekosea umekosea. Kama CCM itaniteuwa mimi staili yangu ni hiyo hiyo."

No comments: