Monday 22 June 2015

zaidi ya Wakazi 20,000 Sengerema kunufaika na mradi wa maji ya bomba.

Zaidi ya wakazi elfu ishirini wa vijiji vya lumeya,kalebezo na nyehunge wilayani sengerema mkoani mwanza wanatarajia kuanza kupata maji ya bomba baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya matenki ya kuhifadhia maji, usimikaji wa mashine ya kusukuma maji na ujenzi wa bomba kubwa la kusafirisha maji kutoka ziwa victoria.

Mradi huo wa maji ya bomba lumeya, kalebezo hadi nyehunge ulioanza kutekelezwa oktoba 2012 na mkandarasi kampuni ya PET COOPERATION LTD ya kahama kwa gharama ya shilingi bilioni moja na milioni mia sita tisini na nne unatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa kwa wananchi ifikapo julai 31 mwaka huu, ambapo kwa mujibu wa mhandisi wa maji wilayani Sengerema Nicas Ligombi kwa sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 90 na upo kwenye hatua ya majaribio.
 
Mbunge wa jimbo la Buchosa ambaye pia ni naibu waziri wa uchukuzi Mh.Dk. Charles Tizeba akizungumza mbele ya katibu mkuu wa chama cha mapinduzi Abdulrahman Kinana ambaye yupo katika ziara ya siku kumi mkoani Mwanza, ametaja baadhi ya changamoto za utekelezaji wa mradi huo ikiwemo kuchelewa kupokelewa kwa wakati fedha za kugharimia mradi huo.
 
Kwa upande wake katibu mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana akizungumza na wananchi baada ya kuona chanzo cha maji kilichopo katika kijiji cha Lumeya amewataka wananchi kutunza na kulinda vyanzo vya maji na kuacha tabia ya kuhujumu miundominu ya maji kwani fedha zinazotumika kugharimia miradi hiyo ni kodi za wananchi.
 
Mradi wa maji wa zamani ulikuwa na uwezo wa kuhudumia wakazi wapatao 2,600 ambapo ulikuwa na vituo 13 vya kuchotea maji,huku pampu ya awali ikiwa na uwezo wa kusukuma lita 33,000 za ujazo kwa saa.

No comments: