Homa ya Uchaguzi Mkuu imeifanya Chadema kuitisha kikao cha dharura cha Kamati Kuu ili kujadili mambo ya kitaifa, ikiwamo adhabu waliyopewa wabunge wa Ukawa kabla ya kutoa tamko.
Kikao hicho kilichofanyika jana, pia kilihusisha
wabunge walioadhibiwa kwa kufanya fujo bungeni wakipinga kuwasilishwa
kwa miswada mitatu ya mafuta na gesi kwa hati ya dharura na hivyo kupewa
adhabu tofauti ya kutohudhuria vikao kuanzia viwili hadi vyote
vilivyosalia.
Wakizungumza na waandishi wa habari, manaibu
katibu mkuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara) walisema
kutokana na kuongezeka kwa homa ya uchaguzi, chama hicho kimelazimika
kuitisha kikao hicho na kwenda tofauti na ratiba yake ya mwaka ili
kuweka sawa baadhi ya mambo.
“Pamoja na ratiba iliyopo, kila litakapokuwa
linajitokeza jambo muhimu tutakuwa tunaitana ili kulijadili kwa kina.
Hali ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura Zanzibar ina
ishara zote kuwa hatutakuwa na mwisho mzuri,” alisema Mwalimu na
kufafanua kuwa kikao hicho kitakuja na jibu... “Kama hali hiyo
haitarekebishwa, upo uwezekano wa athari zake kufika Bara pia.”
Mwishoni mwa wiki, polisi walifyatua risasi kwenye
kituo cha kuandikisha wapigakura baada ya wananchi kwenda eneo hilo
kujaribu kuzuia kile walichokiita “wapigakura mamluki” na kusababisha
watu kadhaa kujeruhiwa na baadhi yao kulazwa hospitalini.
Mwalimu alisema majibu rahisi yanayotolewa na
Serikali kuhusu vurugu hizo kuwa zinafanywa na vikundi vya wahuni,
yanatia shaka hasa kwa kuzingatia kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vipo
na vinashuhudia mambo hayo yakitokea.
Alieleza kuwa matukio yasiyo ya kawaida hayatokei
Zanzibar pekee, bali hata maeneo mengine, akitoa mfano kwenye
uandikishaji wapigakura kwa kutumia teknolojia ya BVR ambako alisema
kuna hali inayokanganya hivyo kufanya kuwapo umuhimu kwa chama kutoa
tamko juu ya kinachoendelea.
“Wale walioandikishwa mwanzo kwenye wilaya za
Mlele mkoani Katavi na Kilombero, Morogoro wameambiwa warudishe kadi
walizopewa na waandikishwe upya. Hii siyo hali ya kawaida na hasa
inafanywa katika majimbo ambayo ni ngome ya Chadema,” alisema na
kuongeza:
“Pamoja na hayo yote, tutatangaza ushindi mapema sana wilayani Kilombero katika uchaguzi mkuu ujao.”
Kuhusu kikao hicho, Mnyika alisema kilijadili
maandalizi ya jumla ya Uchaguzi Mkuu, kupokea taarifa za wagombea
udiwani, ubunge na urais, taarifa ya majadiliano ya Ukawa pamoja na ile
ya wabunge waliopewa adhabu.
Akitoa msimamo wa awali wa chama chake, Mnyika
alisema wabunge hao walikuwa na sababu zote za msingi za kupinga miswada
hiyo na kwamba taarifa zilizoripotiwa kuwa wanatumiwa hazina mashiko
yoyote.
“Chama kinaungana na wabunge wa Ukawa kumtaka Rais
asisaini miswada hiyo. Tunazo taarifa kuwa uharakishaji huu unafanywa
ili kutimiza masharti tuliyopewa na mataifa ya nje ikiwa ni pamoja na
vigezo vya kupata fedha za Mfuko wa Milenia,” alisema Mnyika.
Wakati Chadema ikifanya hivyo, inatarajiwa kuwa vyama vingine
vinavyounda Ukawa vitafanya vikao vyake na kufikia uamuzi ambao
utawasilishwa katika kikao cha wakuu wa vyama hivyo na kujadiliwa.
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Shawej
Mketo alisema jana kuwa pamoja na vikao vya umoja huo, kila chama kina
ratiba yake ya vikao vya ndani.
“Tutakuwa na kikao cha Baraza Kuu na Kamati ya
Utendaji mwishoni mwa mwezi huu. Nadhani ni mara tu baada ya Sikukuu za
Idd. Mambo yote yatajadiliwa huko,” alisema Mketo.
Katibu Mkuu wa NCCR – Mageuzi, Mosena Nyambabe
alisema chama chake kilishafanya mkutano mkuu Juni 27 na uwezekano wa
kuwa na kikao kingine utakuwapo endapo kutakuwa na mgombea urais kutoka
ndani ya chama hicho.
Kuhusu wabunge waliopewa adhabu, Nyambabe alisema
kwa kuwa ndani ya Bunge yumo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye
pia Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pamoja na wa chama
chake, James Mbatia jambo hilo litajadiliwa vizuri katika kikao cha
pamoja.
No comments:
Post a Comment