Wednesday, 8 July 2015

Rais Kikwete Ajiandikisha Kupiga Kura Kwa Kutumia BVR Kijijini Msoga........NEC Yasema Watu Milioni 11 Wamekwisha Jiandikisha Mpaka sasa


Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva amesema hadi sasa wameshaandikisha wapigakura zaidi ya milioni kumi na moja kati ya milioni 24 wanaotarajiwa kuandikishwa nchini kote. 
 
Kutokana na idadi hiyo, Jaji Lubuva amesema NEC ina uhakika wa kukamilisha kazi hiyo ya uandikishaji mapema Agosti mwaka huu.
 
Alisema hayo jana alipokuwa Msoga, Chalinze wilayani Bagamoyo wakati akitoa taarifa kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye alikuwa mmoja wa wananchi wa eneo hilo waliojitokeza kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura, ikiwa ni siku ya kwanza ya kuanza kazi hiyo mkoani Pwani.
 
Alimueleza Rais Kikwete kuwa licha ya changamoto kadhaa zilizojitokeza katika mchakato huo, hali ya uandikishaji ilipofikia nchini hadi juzi ni nzuri na matumaini ya NEC ni kukamilika mapema Agosti kwa kuwafikia walengwa wote waliokusudiwa.
 
Awali, Jaji Lubuva alikuwa akisema kuwa kazi hiyo ingekamilika Julai na hata uandikishaji uliposogezwa mbele kwa jiji la Dar es Salaam na Pwani, NEC ilisisitiza kuwa utakamilika kabla ya mwisho wa Julai.
 
“Mheshimiwa Rais, pamoja na changamoto nyingi na kelele nyingi zilizokuwa zikisikika huku na kule, tayari tumeandikisha watu 11,248,198 mpaka jana (juzi) kati ya lengo tulilojiwekea la kuwafikia watu kati ya milioni 21 mpaka 23 na mikoa iliyokuwa tayari imekamilisha zoezi hili ni 13, bado kumi na moja ambayo nayo nakuhakikishia itakamilisha na mapema mwezi Agosti kazi hii itakamilika,” alisema Jaji Lubuva.
 
Pongezi za Kikwete
Mapema baada ya kujiandikisha, Rais Kikwete aliipongeza Tume kwa hatua iliyofikia hadi sasa na kuitaka isife moyo.
 
Rais Kikwete alibainisha kuwa changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza wakati wa kazi hiyo zichukuliwe kuwa ni fursa ya kuikamilisha kwa wakati.
 
Alitumia mifano ya semi za lugha ya Kiswahili zinazohimiza umakini, akisema “kawia ufike” na “polepole ndiyo mwendo” na hivyo kueleza kuwa Tume ina kila sababu ya kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
 
Rais Kikwete pia alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kujitokeza kujiandikisha ili watumie haki yao kuchagua viongozi wanaowataka kuanzia diwani, mbunge na hata rais na kwamba wasipofanya hivyo, wasije kulalamikia viongozi watakaokuwa madarakani ambao watakuwa wamechaguliwa na wenzao waliojiandikisha. 
 
“Napenda niwakumbushe Watanzania wenzangu, jitokezeni kujiandikisha sasa ili mtumie haki yenu ya kupiga kura kuchagua kiongozi, kama diwani, mbunge au rais mnayemtaka ninyi na siyo uache kujiandikisha halafu usipige kura kisha, uje ulaumu ‘huyu naye vipi anatuongozaje?, mbona hafai?’, huku jibu ulikuwa nalo kama ungepiga kura,” alisema Rais Kikwete.
 
Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete aliyekuwa miongoni mwa wananchi waliojitokeza kujiandikisha aliwataka viongozi na wananchi wahamasishane kujitokeza siku hizi za mwanzoni badala ya kusubiri siku za mwisho.

Diwani wa Kata ya Msoga, Mohamed Mzimba alitaja changamoto zilizopo katika shughuli hiyo kuwa ni kuwapo kwa vituo ambavyo havina umeme na kueleza kuwa halmashauri imelazimika kununua jenereta na kuzisambaza kuhakikisha kazi hiyo haikwami. 
 Afisa TEHAMA kutoka ofisi ya Tume ya Uchaguzi Taifa ya Uchaguzi Bwana Sanif Khalfan akichukua lama za vidole vya Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete wakati Rais alipokwenda kujiandikisha kijijini kwake Msoga wilaya ya Bagamoyo  jana.
 Bwana SANIF Khalfan ambaye ni Afisa TEHAMA kutoka ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi akimpiga picha Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete wakati Rais alipokwenda kujiandikisha kupiga kura kwa kutkumia teknolojia mpya ya BVR kijijini Kwake Msoga  jana.
 Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akiweka saini katika kitambulisho chake wakati wa zoezi la kujiandikisha kijijni kwake Msoga .
 Mwenyekiti wa tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Damian Lubuva akimkabidhi Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete kitambulisho chake cha kupiga kura baada ya Rais Kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia teknolojia ya BVR huko kijijini Msoga wilayani Bagamoyo .
Rais Kikwete akimshukuru Mwenyekiti wa tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Damian Lubuva baada ya kukabidhiwa  kitambulisho chake cha kupiga kura baada ya  kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia teknolojia ya BVR huko kijijini Msoga wilayani Bagamoyo .

No comments: