Wednesday 8 July 2015

Mchungaji Mtikila Atangaza Kuwafikisha Mahakamani Wasaka Urais 6 wa CCM......Yumo Lowassa, Sumaye,Membe,January Wassira na Ngeleja


CHAMA cha Democratic Party (DP) kimetangaza kwenda mahakamani kukishtaki Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na makada wake sita kutokana na kukiuka sheria ya nchi, taratibu pamoja na kanuni za uchaguzi.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa chama hicho Mchungaji Christopher Mtikila, wakati akizungumza na waandishi wa habari. Alisema makada hao pamoja na chama chao wamekiuka sheria za nchi pamoja na kanuni za uchaguzi.

Aliwataja makada ambao atawaburuta mahakamani kuwa ni Mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa pamoja na Frederick Sumaye.
 
Wengine ni January Makamba, William Ngeleja, Stephen Wassira pamoja na Benard Membe. Alidai makada hao walivunja sheria za nchi pamoja na kanuni za uchaguzi kutokana na kuanza kampeni zao mapema.

Alisema  watakishtaki Chama Cha Mapinduzi kutokana na kushindwa kuwachukulia hatua na kuendelea kuwaweka katika mchakato wa kutafuta mgombea wa urais wa chama hicho wakati walishavunja sheria pamoja kanuni za uchaguzi, kwahiyo walitakiwa kukatwa mapema kabisa.

"Watu wameanza kampeni mapema na kwa kufuata sheria ya nchi taratibu  pamoja na kanuni za uchaguzi ni kwamba watu hao wamevunja Sheria kwa hiyo tunapeleka kesi mahakamani kuwashtaki wao pamoja na chama chao kwa kuvunja sheria," alisema Mtikila na kuongeza;

"Tunaenda mahakamani kuishtaki CCM iliyochezea uhuru wetu kwa miaka 54 pamoja na hawa watu wao kwani hawafai na hii nchi inapoelekea ni kubaya."

Alisema uchaguzi wa mwaka huu hautakuwa halali kama sheria hazitafuatwa na kudai kuwa vitu vinavyounyima uchaguzi wa mwaka huu uhalali ni pamoja na watu kuvunja sheria kwa kuanza kampeni mapema.

Alisema inashangaza kuona pesa zinatumika bure bila sababu ya msingi na kudai kuwa ni uhalifu mkubwa tena wa kimataifa. 
 
Alisema watu wanaotumia pesa wakiachwa kitatokea kitu kibaya nchini, hii ni mbaya sana kwani pesa zinazotumika kwa sasa lazima ijulikane zinatoka wapi.

Alisema fedha hizo zinazotumika ipo  siku zitakuja kurudi mahali pake kwa hao watu wanaozitoa.

Aliendelea kusema kuwa inashangaza kuona watu wanatumia pesa  kutafuta urais. Mtikila alimshukia moja kwa moja Lowassa akisema hastahili kupewa nafasi hiyo.

"Lowasa hastahili nafasi hiyo na wanasheria wetu wapo katika maandalizi ya kuandaa kesi kwa ajili ya kuwapeleka mahakamani," alisema Mtikila.

Alisema endapo wataona katika chama chochote kuna vitendo kama ambavyo havifai hawatasita kufuata utaratibu wa kwenda mahakamani endapo watakuwa na ushahidi wa kutosha. 
 
Alisema DP ipo kwenye maandalizi na wakati ukifika watu wote watafikishwa mahakamani.

No comments: