Wednesday 8 July 2015

Pius Msekwa Asema Atakayekatwa Jina na Akaona Ameonewa Anaruhusiwa Kuhama Chama.......Kaongelea Pia Jinsi Escrow Inavyoitesa CCM


Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa amesema kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow imekijengea chama hicho chuki kwa wananchi na hivyo kinahitaji mgombea anayekubalika ili kishinde kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba. 
 
Msekwa, ambaye ni mmoja wa viongozi wa zamani wanaotarajiwa kutoa mapendekezo yatakayokuwa msingi wa kupata mgombea wa urais wa CCM, alisema hayo kwenye kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa kila Jumatatu na Kituo cha Televisheni cha ITV.
 
CCM imeshaanza mchakato wa mwisho wa kumpata mgombea wa urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 kwa ajili ya kuwania kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano na pia mrithi wa Jakaya Kikwete kwenye nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho. 
 
Mchakato huo utakamilika Jumapili wiki hii wakati Mkutano Mkuu utakapochagua mgombea wa nafasi hiyo ya juu ya kisiasa nchini.
 
Akizungumza kwenye kipindi hicho, Msekwa alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, ushindi wa mgombea urais wa CCM, Rais Kikwete, uliporomoka kutoka asilimia 82 hadi 61 kwa sababu kulikuwa na matukio mengi yaliyowafanya wananchi wajenge chuki dhidi ya chama hicho.
 
“Lakini uchaguzi wa mwaka huu, kuna jambo moja tu la escrow,” alisema Msekwa.
 
Msekwa, ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Nane, alisema sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow limejenga chuki na hasira mpya kwa wananchi, hivyo CCM lazima iwe na wagombea wanaokubalika katika jamii.
 
Msekwa alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa kama matukio ya aina mbalimbali yaliyotokea miaka ya nyuma yanaweza kuwa sababu ya wananchi kuwa na chuki na CCM, kukifanya chama hicho kuwa na wakati mgumu katika chaguzi mbalimbali.
 
“Hayo ni maamuzi ya wananchi. Mimi siwezi kutabiri chuki hiyo ni kubwa kiasi gani. Wakati ule chuki ilikuwa kubwa sana na tuliiona hata viongozi wa dini walikasirishwa sana. Hiyo ndiyo ilifanya CCM ipate ushindi wa asilimia 61,” alisema.
 
“Sasa hivi suala lililopo mbele yetu ni escrow tu, hivyo siwezi kupima ukubwa wake ukoje na itatupa ushindi kwa asilimia gani. Ila nina imani kuwa tutashinda lakini sijui ni asilimia ngapi maana inategemea ukubwa wa chuki dhidi ya CCM.”
 
Katika sakata hilo, zaidi ya Sh306 bilioni zilichotwa kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na fedha hizo zilionekana zikiingia kwenye akaunti za baadhi ya mawaziri, wabunge, majaji na watendaji waandamizi serikalini.
 
Sakata hilo lilimlazimu Rais Kikwete kumwengua Profesa Anna Tibaijuka katika wadhifa wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi huku Profesa Sospeter Muhongo, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini sambamba na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, wakilazimika kuachia ngazi.
 
Wizi wa mabilioni hayo uliwekwa wazi katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambayo iliibua mjadala mkubwa bungeni.


Kuhusu mchujo wa kumpata mgombea urais wa CCM mwaka huu, Msekwa alisema hauwezi kukigawa chama licha ya kuwapo kwa makundi mengi yanayowaunga mkono makada tofauti.
 
“Huwezi kuepuka makundi katika uchaguzi kwa sababu hakuna anayetoka nyumbani kwake peke yake na kwenda kutafuta uongozi. Lazima atakuwa na wanaomuunga mkono na muungaji mkono wa kwanza atakuwa mke wake,” alisema Msekwa.
 
Alisema kila mwanachama wa CCM anakula kiapo cha kuwa mwaminifu kwa chama, hivyo anayetafuta uongozi lazima atii uamuzi wa chama na kusisitiza huo ndiyo uaminifu. 
 
“Tunategemea wanachama wetu watatii kiapo chao. Hatuwafungi kamba shingoni. Ambaye ataona hakubaliani na uamuzi atatoka na wamewahi kutoka na waliobaki tukabaki,” alisema Msekwa.
 
Alisema uchaguzi wa mwaka 2010 wapo baadhi ya makada wa chama hicho walijiunga na vyama vya upinzani baada ya kutoswa katika kura za maoni za ubunge CCM.
 
Alisema CCM ni kama maji ya Mto Rufiji, akisisitiza kuwa huwezi kuchota maji yake katika ndoo na kujisifu kuwa umeyamaliza yote... “Maji yatabaki mengi tu. CCM kina mamilioni ya wanachama, wataondoka 10 au 20 lakini wengi watabaki.”

No comments: