Sunday 3 April 2016

MWENYEKITI CHADEMA NA MTENDAJI MBEYA MBARONI 

Na Uncle TOM,MBEYA

HIVI karibuni Wananchi wa kitongoji cha Nsalala,Kata ya Nsalala,katika mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi,mkoani mbeya wamepaza sauti zao katika mkutano wa hadhara uliofanyika Machi,26 mwaka 2016 wakiwatuhumu viongozi wao kuuza shamba lao na kula fedha kiasi cha zaidi ya Sh.Mil.8.6.

Kilio hicho kimemfikia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya,Upendo Sanga ambaye aliamua kuunda Tume kufanya uchunguzi wa awali iliyokuja na majibu kuwa Mtendaji wa kitongoji Lwitiko Mwaibinda na tuhuma sita ikiwemo ya matumizi mabaya ya madaraka na kughushi nyaraka na mihtasari ya vikao.

Akitoa taarifa ya agizo la Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya,Mwanasheria wa halmashauri hiyo Prosper Msivalla amesema Mtendaji wa kitongoji Mwaibinda amekutwa na makosa ya kumndanganya Mwajiri wake kwa kuficha ardhi ya Mamlaka na kutokukabidhi kwa Mamlaka.

Aidha Prosper ametaja tuhuma zinazomkabili Mwenyekiti wa kitongoji Stephano Mshani ni kushiriki kuuza mali ya umma kinyume na taratibu za sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2011 pamoja na kosa la kutunza fedha zilizotokana na mauzo hayo kwenye akaunti zake nambari 6251000804 na akaunti nambari 625160009 zote ktk Benki ya NMB Mbalizi Road.

Baada ya taarifa hiyo Mwenyekiti wa kitongoji Mshani licha ya kuwa mtuhumiwa alisimama na kutoa ufafanuzi kuhusu kufungwa mkutano ambapo Clouds Tv kwa nyakati tofauti imezungumza na wananchi kuhusiana na sakata la viongozi hao ambapo Matatizo Kabenga na Judith Sichone kutoka kituo cha taarifa na maarifa cha Tumaini,Nsalala wamepongeza hatua hiyo.

Diwani wa Kata ya Nsalala,Kisman Mwangomale ameelezea hatua aliyoichukuwa awali baada ya kusikia tetesi ya sakata hilo ambapo Felista Kaisi amemuomba Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbeya kuongeza nguvu katika suala hilo huku Furaha Sanga akisisitiza kuwa wananchi walishirikishwa.

Nimeshuhudia Viongozi hao wakiwa chini ya ulinzi wa Jeshi la polisi na kuchukuliwa na gari la polisi lenye nambari za usajili PT 1836 aina ya Toyota Land Cluiser kuelekea katika kituo cha polisi Mbalizi kwa hatua zaidi ambapo mkutano huo ulimalizika kwa amani licha ya kuwepo vijembe kadhaa kati ya wananchi wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).


No comments: