Kitendo cha aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya pamoja na maofisa wawili waandamizi wa zamani wa Benki ya Stanbic, Tawi la Tanzania, Sioi Solomoni na Shose Sinare kubeba ndoo wakati wakitoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuelekea mahabusu, kimezua maswali mengi.
Kitilya na wenzake hao walifikishwa kwenye mahakama hiyo na kusomewa makosa manane likiwamo la kutakatisha fedha kiasi cha Dola milioni sita za Marekani.
Sinare aliyekuwa mrembo wa Tanzania mwaka 1996, anakabiliwa na mashtaka mengine mawili ya kughushi na mengine ya kuwasilisha nyaraka za uongo za Serikali ya Tanzania ilipokopa Dola za Marekani 550 milioni kutoka Benki ya Standard ya Uingereza kati ya mwaka 2012 na 2013.
Mvutano wa kisheria ulioibuka mahakamani hapo juzi ulimfanya Hakimu Elimius Mchauru anayesikiliza kesi hiyo kuamuru washtakiwa wapelekwe mahabusu hadi Aprili 8, mwaka huu atakapotoa uamuzi kama watuhumiwa hao wana haki ya kupewa dhamana au la.
Wakati wakiondoka kwenda kupanda magari tayari kwa kuelekea gerezani, washtakiwa hao walikuwa wamebeba ndoo ndogo za plastiki. Kitilya alionekana akiwa amebeba ndoo moja, Sioi mbili na Sinare moja.
Ndoo hizo zimezua maswali mengi bila majibu ikiwamo sababu ya kuzibeba, muda uliotumika kuziandaa au kama walikwenda nazo mahakamani wakijua watakosa dhamana na kupelekwa mahabusu.
Pia, maswali yameibuka kuwa walikuwa wakienda nazo mahabusu kufanya nini na je, mahabusi wote huenda na ndoo? Au ni wao tu.
Wakili wa kujitegemea wa kampuni ya uwakili ya Kakamba and Partiners, Mathew Kakamba alisema ameshangaa kuona watuhumiwa wanaelekea mahabusu wakiwa na ndoo.
Alisema hakuna sheria inayoruhusu mtuhumiwa yeyote kwenda na kitu chochote huko na ndiyo maana hufanyiwa upekuzi.
“Ndiyo maana hata mkanda, simu na vifaa vingine wanatakiwa kuviacha mapokezi, sasa sijajua kama hizo ndoo waliruhusiwa kuingia nazo au la,”alisema.
Akizungumzia suala hilo, Ofisa Habari wa Jeshi la Magereza, Lucas Mboje alisema huenda walikuwa wamehifadhia baadhi ya vitu vyao ambavyo wangekwenda navyo mahabusu.
“Labda wamebeba kwa ajili ya kuogea au kuhifadhia baadhi ya vitu vyao lakini kwa Magereza za Dar es Salaam hakuna tatizo la maji,” alisema Mboje.
No comments:
Post a Comment