Wednesday 21 June 2017

TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI

AMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA

                          Ofisi ya Kamanda wa Polisi,                                                                                                                                                                                                   Mkoa  wa  Mbeya,                                                                                   
Namba ya simu 2502572                                                                                               S. L. P. 260,
Fax - +255252503734                                                                                   MBEYA.
E-mail:- rpc.mbeya@tpf.go.tz
              tanpol.mbeya@gmail.com
                                                       

TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI “PRESS RELEASE” TAREHE 21.06.2017.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu.

KUINGIA NCHINI BILA KIBALI [UHAMIAJI HARAMU]

Mnamo tarehe 19.06.2017 majira saa 18:45 jioni, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko Mtaa wa Itanji uliopo Kata ya Iganjo, Tarafa ya Iyunga, Jiji na Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kuwakamata watu wawili ambao ni SEBISIBE MELELE [18] raia wa Ethopia na mwenzake BERISK TAMALIAM [16] raia wa Ethiopia  kwa kosa la kuingia nchini bila Kibali. Taratibu za kuwakabidhi Idara ya Uhamiaji kwa hatua zaidi za kisheria zinaendelea.

KUPATIKANA NA POMBE MOSHI [GONGO]

Mnamo tarehe 20.06.2017 majira ya saa 12:45 Mchana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko Mtaa wa Mwanyanje, Kata ya Iganjo, Tarafa ya Iyunga, JIji na mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kumkamata mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la  FREDINA MWAIJANDE [32] Mkazi wa Iganjo akiwa na Pombe Haramu ya Moshi [Gongo] ujazo wa lita 4. Mtuhumiwa ni muuzaji wa Pombe hiyo na mara baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa mahakamani.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa mahala salama. Hata hivyo kumekuwa na tukio 01 la mauaji na taarifa 01 ya kifo kama ifuatavyo:-

Mnamo tarehe 20.06.2017 majira ya saa 23:00 usiku huko katika Klabu cha Pombe za Kienyeji kiitwacho “Mande” kilichopo Kijiji cha Isangala, Kata ya Iwindi, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Kipolisi Mbalizi, Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la MATOKEO AMON MWANYULA [30] Mkazi wa Kijiji cha Isangala alikutwa ameuawa kwa kukatwa panga kichwani na mtu/watu wasiofahamika.

Chanzo cha tukio bado hakijafahamika. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Ifisi kwa uchunguzi wa kitabibu. Upelelezi unaendelea.

Mnamo tarehe 19.06.2017 majira ya saa 09:00 Asubuhi huko Kitongoji cha Katumba, Kijiji na Kata ya Mababu, Tarafa ya Ntebela, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la FURAHA MORNING [38] Mkazi wa Katumba alikutwa amekufa maji katika Mto Kipake.

Inadaiwa kuwa, marehemu alitoka nyumbani kwake na kuelekea mtoni kwa ajili ya kufua nguo zake kando kando ya Mto huo na kutumbukia kisha kuzama kwenye kina kirefu cha Mto hali iliyopelekea kunywa maji mengi.

Kabla ya tukio hilo, marehemu alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kifafa hali inayodaiwa kusababisha kudondoka na kutumbukia katika Mto huo. Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kitabibu na kukabidhiwa ndugu kwa ajili ya mazishi.

WITO:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa jamii kuacha kutumia Dawa za Kulevya kwani ni kinyume cha sheria na ni hatari kwa afya ya mtumiaji. Aidha Kamanda KIDAVASHARI anatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za mtu/watu waliohusika katika tukio la mauaji kutoa taarifa Polisi ili watuhumiwa wakamatwe kwa hatua zaidi za kisheria. Aidha anatoa wito kwa wananchi, kufunika visima vilivyowazi, kufukia mashimo yaliyojaa maji kutokana na mvua zilizonyesha kwani ni hatari kiusalama hasa kwa watoto wadogo.

                                               Imesainiwa na:
[DHAHIRI A. KIDAVASHARI - DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA

No comments: