Tuesday, 9 July 2013

KIBOKO YA KAVUMBANGU ATUA LEO DAR KUJIUNGA NA SIMBA SC



MFUNGAJI bora wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka huu, Amisi Tambwe wa Vital’O ya Burundi amewasili leo mjini Dar es Salaam kwa ajili ya kujiunga na klabu ya Simba SC ya Jijini kwa msimu ujao.
Tambwe ameiongoza Vital’O kutwaa taji la kwanza la Kagame mwaka huu katika michuano iliyofanyika nchini Sudan na pia akiibuka mfungaji bora wa mashindano hayo kwa mabao yake sita.
Kifaa kipya chaja Msimbazi; Tambwe aliyenyanyua Kombe la Kagame akiwa na wachezaji wenzake wa Vital'O hivi karibuni nchini Sudan 

Na huyo pia ndiye mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Burundi na mshambuliaji chaguo la kwanza katika timu ya taifa ya nchi hiyo, Int’hamba Murugamba, ambaye anamfanya mchezaji wa Yanga, Didier Kavumbangu awe nje ya kikosi.  
Tambwe aliyefunga mabao 28 msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Burundi, ametua asubuhi ya leo kwa basi kutoka kwao Bujumbura na ataisubiri timu hiyo iliyopo ziarani Katavi irejee Dar es Salaam ili ajiunge nayo kwa mazoezi.
Tambwe anakuja akiwa na nafasi kubwa ya kusajiliwa moja kwa moja Simba SC, wakati tayari kuna mshambuliaji kutoka Sudan Kusini, Kon James kutoka klabu ya Al Nasir Juba amekuja kufanya majaribio.
Tambwe anakuwa mchezaji wa nane katika orodha ya wachezaji wa kigeni wanaowania nafasi tano za kuwamo kwenye kikosi cha Simba SC msimu ujao, wengine wakiwa ni Waganda kipa Abbel Dhaira, mabeki Samuel Ssenkoom, Assumani Buyinza na kiungo Mussa Mudde pamoja na washambuliaji Felix Cuipoi kutoka DRC na Kon James kutoka Sudan Kusini.
Dhaira na Mudde wapo tangu msimu uliopita, wakati Ssenkoom, amekuja kutoka URA ya kwao, Buyinza ametoka Vietnam na Cuipoi alikuwa anacheza Cameroon.

No comments: