MICHUANO ya kombe la Muungano
inayofanyika wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, imeendelea leo katika
kituo cha Igowole ambapo wakali kutoka jijini Mbeya, klabu ya Mbeya City
wameshuka dimbani dhidi ya Zamalek ya Njombe. (HM)
Katika mchezo huo, Zamalek wamecharazwa bao 1-0, hivyo Mbeya City kunyemelea uongozi wa kituo hicho.
Mratibu wa mashindano hayo ya
kihistoria ambayo yalimtoa kisoka mshambuliaji nyota wa zamani wa Simba ,
Taifa Stars na sasa Prisons ya jiji Mbeya, Emmanuel Gabriel Mwakyusa,
Daud Yasin amezungumza na FULLSHANGWE na kusema kuwa mchezo huo ulikuwa mkali sana kwani timu zote zilionesha kiwango cha hali ya juu.
“Kadri siku zinavyozidi kwenda
michuano inanoga zaidi, leo hii kipute kilikuwa kikali zaidi na umepigwa
mpira wa kiwango cha juu sana na kuwaacha hoi mashabiki waliofurika
kutazama kabumbu safi”. Alisema Yasin.
Yasin alisema ingawa kuna changamoto
kubwa ya udhamini katika mashindano hayo, lakini mambo yanazidi kuwa
mazuri kufuatia timu zote kuonesha ushindanii mkubwa na kuibua hamasa
kubwa ambayo haijawahi kutokea kwa mashabiki wa soka mkoani Iringa.
Kwa upande wa kocha wa Mbeya City Maka
Mwalwisyi amesema kikosi chake kimecheza vizuri licha ya kukabiliwa na
changamoto kubwa kutoka kwa Zamalek.
“Tunamshukuru Mungu mchezo
umemalizika, tumecheza vizuri na vijana walizingatia maelekezo yangu na
ndio maana mambo yamekwenda kama nilivyotarajia”. Alisema Mwalwisyi.
Kocha huyo alisisitiza kuwa nia yake ni kuwaa ubingwa wa michuano hiyo ambayo inafanyika kwa mwaka wa 17 sasa.
“Ubingwa haunitoki mwaka huu, upinzani
ni mkubwa sana, lakini nimejipanga kupambana kwa hali zote ili kurudi
na taji nyumbani”. Alisema Mwalwisyi.
Kesho ni mapumziko na michuano hiyo itaendelea kushika kasi kesho kutwa. Chanzo: Baraka Mpenja
No comments:
Post a Comment