Saturday, 28 September 2013

auawa na Bibi yake kwa kuchelewa kuleta Mwiko wa Ugali

DSC03304 3589a

Mtuhumiwa Magreth Sombi anayetuhumiwa kumuua mjukuu wake Zuhura
Na Nathaniel Limu, Kiomboi
Mtoto wa kike aliyetambulika kwa jina moja la Zuhura (6) mkazi wa mtaa wa Lulumba New Kiomboi mjini, wilayani Iramba,amefariki dunia baada ya kudaiwa kuuguzwa kwa maji ya moto na bibi yake Magreth Sombi (55).(hd)
Imedaiwa kwamba Zuhura alimwagiwa maji ya moto ambayo yalikuwa yatumike kupikia ugali,kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kitendo cha mtoto huyo kuchelewa kukabidhi mwiko aliotumwa na bibi yake.
Akisimulia mkasa huo wa aina yake,Mwenyekiti wa mtaa wa Lulumba,Abel Seit,amesema tukio hilo limetokea Septemba 24 mwaka huu majira ya jioni huko mtaa wa Lulumba katika mji wa New Kiomboi.
Amesema siku ya tukio,Zuhura alitumwa na bibi yake Magreth akalete mwiko wa kusoga ugali wa jioni na inadaiwa kwamba mtoto huyo alichelewa kuukabidhi mwiko huo.
Seit amesema baada ya kuleta mwiko huo,alimwagiwa mwilini maji yaliyokuwa yamechemka tayari kwa kutumika kupikia ugali wa jioni.
"Kama vile adhabu hiyo haikutosha,Magreth kwa ushirikiano na mtoto wake Naomi,walimkamata kwa nguvu Zuhura na kisha kuingiza viganja vyake vya mikono yote ndani ya sufuria iliyokuwa ina maji yaliyokuwa yamechemka kwa kiwango cha juu.Mtoto Zuhura aliweza kuugua na nyama zote kutoka na kubakia mifupa"amesema kwa masikitiko mwenyekiti huyo.
Seit amesema Zuhura alifariki dunia Septemba 25 akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Iramba.
"Baada ya muda mrefu kupita baada ya Zuhura kufariki dunia,bibi yake Magreth alimtuma mtoto wake Naomi kuja nyumbani kwangu kunipa taarifa hiyo.Cha ajabu ni kwamba hawakupiga yowe wala kutoa taarifa kwa majirani zao",amesema na kuongeza;
"Nilipomhoji ni kwa nini hajawajulisha majirani zao juu ya kifo hicho,kwanza alinionya kwamba nisije nikawaambia watu wala majirani kwa sababu hataki watu wajue au waje warundikane kwake na kwamba mwili wa Zuhura wakati wo wote utachukuliwa na wazazi wake kwenda kuzika Singida mjini".
Kwa upande wake jirani wa karibu wa Magreth,Elieza Mgwali,amesema Zuhura ambaye ana miezi miwli toka aanze kuishi na bibi yake,aliishi kwa mateso makubwa.
"Mtoto huyu ameteseka mno toka aanze kuishi na bibi yake,alifanyishwa kazi ambazo ziko nje ya uwezo wake na mara nyingi alikuwa akinyimwa hata chakula.Mara nyingi tu tulikuwa tunashitukia anaingia kwetu na kwenda moja kwa moja jikoni na kujichukulia chakula bila hata kuomba.Kwa sababu tuliisha tambua mateso yake,tulikuwa tukimruhusu ale hadi ashibe",alisema.
Majirani wa Magreth wamepigwa butwaa kutokana na kitendo hicho kufanywa na mama ambaye alikuwa hakosi kanisani na alikuwa mwimbaji mzuri wa kwaya."Kumbe chui aliyekuwa amevaa ngozi ya kondoo",alisikika mama mmoja ambaye alidai kuwa walikuwa wakisali na Magreth.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa mtaa,Magreth na mtoto wake Naomi,wanashikiliwa na polisi kuhusiana na mauaji hayo.
Juhudi kubwa zimefanywa na mwandishi wa habari hii kupata undani wa mauaji hayo,hazijaa matunda baada ya kumpigia Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida kupitia namba yake ya simu ya mkononi kuita bila kupokelewa na hata meseji ilipotumwa nayo haikuweza kujibiwa:CHANZO MO BLOG

No comments: