Thursday 24 July 2014

MHASIBU WA HALMASHAURI YA WILAYA YA MBEYA KIZIMBANI KWA UBADHILIFU WA SHILINGI MILIONI 1,350,000/=.

MKURUGENZI WA CHUO CHA ILEMI POLYTECHNIC KILICHOPO MBEYA MJINI, ANATANGAZA NAFASI ZA MASOMO 2011.           

 
TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mbeya, imemfikisha mahakamani Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa kosa la kuhujumu uchumi na Rushwa.
 
Mtumishi huyo alifikishwa jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, James Mhanusi chini ya Mwendesha mashtaka wa Takukuru, Nimrod Mafwele.
 
Mwendesha mashtaka wa Serikali Nimrod Mafwele alimtaja mshtakiwa kuwa ni Geshon Bwile ambaye ni mhasibu wa Halmashauri hiyo akituhumiwa kwa makosa matatu aliyoyatenda Mei 2, 2013.
 
Aliyataja makosa hayo kuwa ni pamoja na kutumia Nyaraka za Serikali kujipatia fedha kinyume cha kifungu cha 22 cha Sheria ya Takukuru namba 11 ya mwaka 2007.
 
Alisema katika kosa hilo Mtuhumiwa akiwa ni mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya alitumia risiti yenye namba 0009 kumwandikia Rich & Mr&Mrs Mufat Decoration kwa malipo ya mapambo yenye thamani ya shilingi Milioni 1,350,000 wakati sio kweli.
 
 Mwendesha mashtaka huyo alilitaja kosa lingine kuwa ni Ubadhilifu  kinyume cha kifungu cha 28(1) namba 11 cha mwaka 2007 ambapo alijipatia kiasi cha shilingi Milion 1,350,000 alichokabidhiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.
 
Alilitaka kosa la tatu kuwa ni kuisababishia hasara mamlaka  kinyume cha Sheria kifungu cha 10(1),(i),57(1) na 60(2) ya uhujumu uchumi namba 200 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002, ambapo Halmashauri ilipata hasara ya shilingi Milion 1,350,000 mali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
 
Baada ya kusomewa mashtaka yote hayo Mtuhumiwa alikataa yote ambapo upande wa mashtaka ulisema upelelezi umekamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kusikiliza maelezo ya awali.
 
Aidha mshtakiwa aliachiwa kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ambayo ni kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa Serikali wakiwa na barua kutoka kwa mwajiri,mali kauli ya Shilingi Milioni Moja kila mmoja.
 
Hakimu Mhanusi alisema mashariti mengine ni kutokana na kifungu cha 148 (6) ambapo mtuhumiwa harusiwi kutoka nje ya Mkoa wa Mbeya bila ruhusa ya mahakama pamoja na kuwasilisha hati ya kusafiria kwenye kituo cha polisi jambo ambalo aliyatimiza papo hapo.
 
Hata hivyo kesi hiyo iliahirishwa hadi Julai 25 mwaka huu ambapo mtuhumiwa ataanza kusomewa maelezo ya awali na kuendelea kusikiliza upande wa mashahidi.
 

Kesi hiyo ni ya pili kwa TAKUKURU Mkoa wa Mbeya kuwafikisha Mahakamani watumishi wa Halmashauri ya Mbeya baada ya hivi karibuni kumfikisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Upendo Sanga, na Watumishi wengine kwa kosa la kuhujumu uchumi.

No comments: