Uvumi kuhusu mwanamke mwizi wa nyanya kushindwa kutua tenga umesababisha
polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi mjini Mbalizi
mkoani Mbeya.
Hali ya taharuki imewakumba wananchi wa mji mdogo wa Mbalizi leo
Jumatano baada ya mtu au watu wasiojulikana kuvumishwa kuwa mwanamke
huyo baada ya kushindwa kutua tenga alikimbilia kituo cha Polisi Mbalizi
kuomba msaada.
Uvumi huo ulieleza kuwa, mwanamke huyo aliimba nyanya sokoni Mbalizi.
Katika tukio hilo Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi
kuwatawanya wananchi waliovamia kituo hicho ili kumuona mtuhumiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga amesema uvumi huo
ulienezwa na watu au mtu asiyejulikana kwamba kuna mwanamke aliiba tenga
la nyanya sokoni Mbalizi lakini alipojaribu kulishusha kutoka kichwani
ilishindikana, hivyo akaamua kwenda kituo cha polisi kuomba msaada.
“Wakati wa taharuki kama ile kila mtu anakuwa na tabia na nia yake,
ndiyo maana imelazimika kutumia nguvu kidogo kuwanyamazisha watu kwa
mabomu. Ule ni uvumi tu ambao hata hatujamfahamu aliyeeneza alikuwa na
mlengo gani kwa kuwa hakuna tukio kama hilo,” amesema.
Kamanda Mpinga amesema sasa hali ni shwari na wananchi wameelimishwa
wakaondoka kwenda sehemu zao za biashara na shughuli nyingine.
Mwenyekiti wa Soko la Mbalizi A ambako kituo cha polisi kipo, Geofrey
Msigwa amesema hakuna kitu kama hicho bali naye aliona watu wengi
wakielekea kituoni jambo lililosababisha polisi kuwatawanya kwa mabomu.
Amesema, “Hii ni hatari kwa mtu kusikia jambo bila kulifanyia utafiti na
kuanza kulizusha bila kutambua athari inayoweza kutokea.”
Amelaani kitendo hicho akisema kinahatarisha usalama na amani.
Pia, amewaonya watu kutokimbilia vitu ambavyo ni vya kusikia bila kuvifanyia uchunguzi kwa kuwa inaweza kuwagharimu.
Msigwa amesema hawana taarifa za wizi huo na wanashangazwa na uvumi huo.
Credit: Malunde 1
Credit: Malunde 1
No comments:
Post a Comment