Monday, 19 January 2015

PROF. MWANDOSYA NA UTATU WA SIASA ZA MBEYA


Prof. Mark Mwandosya
NA GORDON KALULUNGA
SIASA za mkoa wa Mbeya, zina historia kubwa sana. Historia hiyo haimwachi mbali, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya kwa miaka 15, Patrick Nswilla, John Mwakangale, mzee Mwambulukutu na Waziri asiye na wizara maalum ofisi ya Rais, Prof. Mark James Mwandosya.
Kiongozi huyu ni Mbunge wa Jimbo la Rungwe Mashariki, lililopo katika Halmashauri ya Busokelo mkoani hapa.
Kwa mkoa wa Mbeya kwa wanasiasa waliopo ndani ya mfumo wa siasa za mkoa huu, yeye ndiye mwanasiasa anayeheshimika zaidi kutokana na hulka yake ya kutabasamu na watu wa rika zote na hasa kuwa mmoja ya viongozi ambao walianza kuthubutu kuwania nafasi ya rais mwaka 2005.
Baadhi ya wananchi wa mkoa wa huu, wanamwita Prof. Mwandosya Baba wa siasa za mkoa wa Mbeya.
Heshima hiyo inatokana na yeye kuwa kiongozi wa NEC mkoa wa Mbeya, ambao aliupata baada ya mchuano mkali kati yake na Kijana Thom Mwang’onda mwaka 1997,  kisha kuibuka mshindi.
Akawa kiongozi mwenye heshima kubwa kwa siasa za Mkoa wa Mbeya, kabla hajakengeuka na kujisahau kutohudhuria vikao vya chama chake, mkoa wa Mbeya.
Wakati baadhi wakiendelea kumpa heshima yake, baadhi ya waliokuwa wapambe wake mwaka huo, hawataki hata kumsikia kutokana na madai kuwa baada ya uchaguzi kuisha hakuweza kuwakumbuka hata kwa salaam na wakawa wanabezwa na kundi la Thom Mwang’onda.
Mmoja ya wapambe wa Prof. Mwandosya anayesikika mara kadhaa na kudai kuwa hajawahi kuthaminiwa baada ya ushindi ni aliyekuwa diwani wa kata ya Utengule Usongwe, Mwalimu Jackob Mwakasole, ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Kanisa la Uinjilisti Tanzania, lenye makao makuu mjini Mbalizi, wilaya ya Mbeya.
Mwingine ambaye licha ya kumkataa kwa muda mrefu, lakini kwa sasa analitangaza vema jina la Prof. Mwandosya na kuamini kuwa akiteuliwa kuwania nafasi ya Rais kupitia CCM,  atakuwa kiongozi bora, ni Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Mbeya, Bashiu Madodi.
Kwa wafuatiliaji wa masuala ya siasa kwa mkoa wa Mbeya, Prof. Mwandosya anaendelea kukumbukwa kwa umahili wake wa kusimamia na kuhakikisha miradi kadhaa inakamilika bila upendeleo, bali kwa kufuata taratibu za serikali.
Anakumbukwa kwa kusimamia kidete uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe ambao umekamilika katika wilaya ya Mbeya, Jimbo la Mbeya Vijijini.
Inaelezwa kuwa, asingekuwa Mwandosya uwanja huo wa ndege ungeenda kujengwa mikoa ya Kaskazini, ingawa haikuwa dhamira ya serikali.
Mbali na uwanja huo wa kimataifa, pia anaendelea kukumbukwa kupigania adhima ya serikali kukifanya chuo cha ufundi MIST kuwa chuo kikuu cha Sayansi na teknolojia(MUST), kilichopo Iyunga Jijini Mbeya.
Sanjari na miradi hiyo mikuu miwili, pia mradi mkubwa wa maji, ambao ulizinduliwa Julai,2012 na Rais Jakaya Kikwete, jina la uongozi uliotukuka wa Prof. Mark Mwandosya, linasadifu.
Prof. Mwandosya ni mmoja kati ya viongozi ambao wanatajwa kuwania nafasi ya rais mwaka huu, kupitia chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Rais Jakaya Kikwete, anao mtihani mkubwa katika uteuzi kama kweli ataangalia suala la urafiki. Edward Lowassa rafiki yake, Benard Membe rafiki yake, January Makamba kijana wake, Mwigulu Nchemba kijana wake, Mizengo Pinda rafiki yake na Prof. Mwandosya ni rafiki yake.
Ni mara chache ambazo Rais Kikwete amefanya ziara mkoani Mbeya bila kuambatana na Prof. Mark Mwandosya na hata katika matembezi ya sherehe za miaka 37 za CCM zilizofanyika mwaka jana 2014, mkoani Mbeya, alikuwa na Prof. Mwandosya na kiongozi huyo aliutangazia umma kuwa kwa sasa amepona na anamshukuru sana Rais Kikwete kwa kumtibu.
Kauli hiyo, ilihisiwa na wachambuzi wa masuala ya siasa kuwa ni salamu tosha kwa wawania nafasi ya rais mwaka huu 2015, ukizingatia kuwa kiongozi huyo alishika nafasi ya tatu mwaka 2005 katika mbio hizo za urais, ambapo kambi yae kubwa ilikuwa kanda ya Ziwa na sasa kambi yake imeongezeka katika kanda ya Nyanda za juu kusini.
Mbali na mapungufu ya Mwandosya kwa wanasiasa wa mkoa wa Mbeya, hasa yanayotokana na hasira za baadhi ya wapambe wake wa mwaka 1997 kwenye nafasi ya NEC, kiongozi huyu anaonekana kurejesha imani kwa kiasi kikubwa kwa baadhi ya wajumbe wa Halmashuri kuu ya Taifa waliopo mkoani Mbeya na Nyanda za juu kusini.
Wajumbe hao, awali baadhi yao walikuwa wakijinasibu kuwa ni wapiga kura watiifu wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, lakini wamebadili msimamo baada ya kile wanachodai kuwa wanaridhishwa na propaganda za kwamba wapambe wa Lowassa, wanawatembelea baadhi ya watu huku wao wakiwa wanatengwa, hivyo kuona kama kambi hiyo imejaa matapeli na hivyo ni bora kuwa wapiga kura huru.
Baadhi ya wajumbe hao, wanasema kuwa, nafasi za kura walizonazo ni tatu, hivyo moja ya kura zao itaangukia kwa Prof. Mwandosya kati ya majina matano ambayo yatapelekwa kwenye kikao chao na kamati kuu.
Baadhi ya watanzania hofu yao ni kwamba, dunia kwa sasa inapigana kuhusu suala la uchumi, je nani kati ya waliojitokeza anaweza kumudu kusimamia rasilimali za Tanzania kwa uadilifu na kukataa kuwa kibaraka wa ‘’viranja’’ wa dunia? Je ni Prof. Mark Mwandosya ataweza kutimiza adhima ya watanzania au kuendelea kuwaunganisha wananchi wa Mbeya?
Nawaasa viongozi wa CCM hasa wale wenye kura za maamuzi, kuwaletea watanzania mgombea anayeweza kuangalia uchumi wa dunia unakoelekea na namna mataifa yanavyochukua umiliki wa uendeshaji wa shughuli muhimu za kiuchumi kisha ajiulize kuwa je hii si sehemu ama aina mpya ya ujamaa?
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere angekuwepo leo hii angesemaje? Hakuna mwenye jibu sahii lakini kwa kuwa alishaonya kwenye hotuba zake, ninaloweza kuhisi ni kuwa angekumbusha kile alichowahi kusema, ambacho wengi hawakudhani kuwa kingetimia na ungekuwa wakati wa kudhihirika tena kwa maono yake.
Mwandishi anapatikna kwa simu 0754 440749 na makala haya inapatikana katika gazeti la MTANZANIA TAREHE 18/01/2015

No comments: