Jana klabu ya Azam FC ilitangaza
rasmi kumsajili mshambuliajii wa Mtibwa Sugar Ameh Ally ‘Zungu’ ili
kukitumikia kikosi cha wana-lambalamba wa Chamazi kwa msimu ujao. Zungu
amesaini mkataba wa miaka miwili kukipiga na Azam na yuko tayari kuanza
majukumu yake mapya muda wowote kuanzia sasa kutokana na kila kitu
kinachohusu usajili wake kukamilika.
Afisa Habari wa Azam FC Jafar Idd
Maganga amesema, Ameh Ally amesajiliwa ikiwa ni moja kati ya wachezaji
watano wa ndani ambao wanataka kuwasajili kwa ajili ya kuimarisha kikosi
chao ili kupambana na michuano inayowakabili msimu ujao.
“Tumeweza kufanya usajili kwa
kumchukua mchezaji kutoka kwenye klabu za ndan,i kama unakumbuka tangu
usajili umeanza watu wamekuwa wakifanya usajili wa watu mbalimbali wa
klabu za ndani lakini sisi tulikuwa kimya kwa muda mrefu, kwa hiyo
tulikuwa tunaangalia tunakwenda wapi, maana mchezo wa usajili ni mchezo
mchafu, ukikosea tu jinsi ya kusajili basi umeua timu kwa msimu mzima.
Kwahiyo leo kwa mara ya kwanza tunatangaza katika wachezaji wa ndani
tumemsajili Ameh Ally kutoka klabu ya Mtibwa”, amesema Maganga.
“Mazungumzo yamekwenda vizuri
kati ya uongozi wa klabu ya Mtibwa na mchezaji mwenyewe, kwahiyo rasmi
mchezaji huyo tumemsaini kwa mkataba wa miaka miwili na ataitumikia Azam
Football Club kwa kipindi kinachofuata”, ameongeza.
“Kama nilivyozungumza siku za
nyuma, hatutakuwa na mabadiliko makubwa sana kwenye timu tunawachezaji
ambao ni ‘local’ hawatozidi watano kwenye timu yetu ambao tutaweza
kuwaongeza kwenye timu kwa maana ya ku-shape timu na kutafuta wachezaji
ambao watakuja kuisaidia timu, sio unatafuta mchezaji ambaye anakuja
kuwa mzigo kwenye timu. Mchezaji ambaye anakuwa kwenye benchi muda wote
kwa maana yule aliyepo ana afadhali kuliko aliyesajiliwa”, amefafanua.
“Tupo makini sana kwenye hilo,
uongozi upo makini sana kushirikiana na benchi la ufundi kuhakikisha
kwamba tunasajili watu ambao wanakuja kuisaidia timu na sio kuja kukaa
kama mizigo kwenye timu kwa maana kuja kukaa benchi au wengine hata
benchi wanashindwa kukaa kwenye wachezaji 16 wanaocheza kwa siku hiyo”,
ameongeza.
“Kwahiyo tumemtangaza Ameh Ally
aliyekuwa akifatiliwa kwa muda mrefu na benchi la ufundi la timu yetu
kuangalia performance yake, sasahivi wamejumuika nae hivyo wameongea na
uongozi umetimiza kile ambacho benchi la ufundi limekitaka. Lakini sisi
hatuna utaratibu wa uongozi kumsajili mtu wanaemtaka bali anasajiliwa
mtu kutokana na benchi la ufundi kutaka. Mchezaji huyo alihitajiwa na
timu yetu. Tumeanza na Ameh Ally wengine watafuata na tutakupeni
taarifa”, amesema Maganga.
“Wageni wetu (makocha na viongozi
wengine) wamewasili na tulikuwa nao kwenye uwanja wa Azam Complex
kuweza kuona eneo lao la kazi na wamefurahia mazingira mazuri wametoa
ushauri wao kitu gani kiongezwe na vinavyofaa ni vitu vya aina gani kwa
hiyo tunashukuru tunakwenda vizuri. Tarehe 15 Juni tunaanza rasmi
kuingia katika viwanja vya Azam Complex kuanza mazoezi kwa maana
tunamashindano ya Kagame, lakini vilevile tuna ligi kuu Tanzania bara”.
“Stewart Hall ni kocha ambaye
anafahamu mazingira ya timu yetu, anafahamu wachezaji kwahiyo, mazoezi
yataanza kwa wale ambao hawako kwenye timu ya Taifa na baadae wale
waliopo kwenye timu ya Taifa watakapokuja wataungana na wenzao kuendelea
na mazoezi kwa pamoja”, Maganga alimaliza.
No comments:
Post a Comment