Wakati maandalizi kwa ajili ya
msimu ujao yakiendelea, timu ya Maimaji ‘Wanalizombe’ wa Songea ambao
wamepanda daraja kucheza ligi kuu Tanzania bara kwa msimu ujao, katibu
mkuu wake Zacharia Ngalemanayo ameamua kung’atuka kuipisha nafasi hiyo
kwa kile alichokieleza kuwa amezidiwa na majukumu ya kifamilia pamoja na
majukumu mengine binafsi.
Ngalemanayo aliwasilisha barua
kwa mwenyekiti wa klabu ya Majimaji akieleza sababu zilizopelekea aamue
kujiuzulu, lakini moja ya sababu ambazo zimeonekana kuwa ni kubwa ni ile
ya kukabiliwa na majukumu ya familia pamoja na majukumu binafsi. Barua
hiyo ambayo iliwasilishwa kwenye kikao cha bodi ya timu hiyo na
mwenyekiti wa timu Humphrey Milanzi, baada ya wajumbe kutafakari kwa
kina juu ya uamuzi huo waliridhia uamuzi wake na kutoa jukumu jingine
tena kwa mwenyekiti ili kuona ni namna gani ya kufanya uteuzi wa katibu
wa klabu hiyo.
Kwa kulingana na majukumu ambayo
klabu ya Majimaji inayo kwa sasa ikiwa ni pamoja na kusajili wachezaji
na kufuatilia taarifa mbalimbali kutoka shirikisho la soka nchini,
mwenyekiti aliwasilisha jina jingine la mtu ambaye amekiri kuziba pengo
hilo ambaye ni Charles Mchanakutwa.
Hivyo kinachosubiriwa hivisasa
ndani ya klabu ya Majimaji ni makabidhiano ambayo yatafanyika muda
wowote kuanzia sasa kwasababu barua hiyo ya kujiuzulu kwa katibu huyo na
jina jipya tayari limeshapelekwa kwenye bodi ya klabu na bodi hiyo
imeridhia.
Majimaji imerejea kunako ligi kuu
ya Tanzania bara msimu wa 2015-2016 baada ya kuporomoka daraja na
kusota kwenye ligi daraja la kwanza kwa misimu kadhaa. Ligi kuu msimu
ujao itakuwa na timu 16 badala ya timu 14 zilizoshiriki ligi
iliyomalizika hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment