Monday 13 July 2015

Mwenyekiti ACT-Wazalendo Azomewa Ukerewe


KATIBU  wa  Chama  cha  ACT- Wazalendo  Mkoa wa  Mwanza,  Robart  Gwanchele, juzi alijikuta katika  wakati  mgumu baada ya wananchi   kumzomea  wakati  akihutubia  mkutano wa  hadhara  mjini Nansio. 

Wananchi  hao walimzomea baada ya Gwanchele kuanza kuwashambulia madiwani na wabunge wa Chadema  kwamba licha ya kuongoza jimbo hilo miaka mitano, bado wameshindwa kutatua kero za wananchi.
 
Sauti za wananchi kuanza kumzomea zilianza chini chini huku wengine wakipaza sauti zao kwa kumtaka aeleze sera za ACT-Wazalaendo na si kuwakashifu viongozi wa Chadema.
 
Gwanchele  alizidi kuwahoji wananchi ndipo alipokumbana na zomea zomea uwanja mzima.
 
Alisema ,  “Nyinyi   mwaka 2010 mlichagua  mbunge na  madiwani wa Chadema   mbona  barabara hazipitiki?  Mnaendelea  kukabiliwa na  tatizo la  maji     mjini  Nansio.
 
“Nyinyi  sikilizeni  tuwaeleze  ukweli  viongozi wenu wameshindwa  kuwaletea maendeleo  na mnaendekeza  siasa za  ushabiki.   Kubalini kwamba  Mbunge wa jimbo hili,  Salvatory Machemli  ameshindwa  kujenga hoja bungeni  na kuondoa  tatizo la  usafiri  wa  meli  kati  ya  Ukerewe na Mwanza,”alisema.

Kauli yake hiyo iliongeza hasira kwa wananchi ambao walimzomea huku wengine wakipiga miluzi na kusababisha  baadhi ya wananchi  kuondoka kwenye mkutano huo.

Hata hivyo Gwanchele aliendelea kuzungumza   na kuwaomba wananchi kukiunga mkono ACT-Wazalendo katika uchaguzi mkuu ujao kwa kuwachagua viongozi wake watakaosimamishwa kuanzia udiwani, ubunge na urais.

Awali, Mwenyekiti wa  ACT-  Wazalendo  wa  Wilaya  ya  Ukerewe, Charles  Mugunda, alisema chama chao kimejipanga kuchukua dola.

No comments: