Thursday, 9 July 2015

RAIS KIKWETE AFICHUA SIRI YA KUACHA KWENDA UWANJANI; “NILIAMBIWA NIKIENDA TIMU INAFUNGWA”

Na: Ipyana Mwankenja, Dodoma.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kwamba aliacha kwenda kwenye mechi za timu ya taifa, Taifa Stars baada ya kuambiwa akienda inafungwa.
Akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma leo kabla ya kulivunja, Rais Kikwete alisema kwamba pamoja na kuacha kwenda kwenye mechi hizo, bado timu haifanyi vizuri. 
“Timu yetu ya taifa haifanyi vizuri, tulianza vizuri na nikawa ninaenda uwanjani pale navaa na jezi,
baadaye wakaniambia, mzee wewe ukija timu haifanyi vizuri, nikaona hawa sasa wanataka kusema mimi nina mkosi,”. 
“Nimeacha kwenda katika mpira, lakini bado hawafanyi vizuri. Hata wakibadilisha mji na kwenda Unguja wanafungwa tatu. Mimi sina tatizo, tatizo ni wao wenyewe,”amesema Rais Kikwete.
Rais huyo kipenzi wa Tanzania amesema lazima Watanzania wajiulize sababu ya matokeo mabaya ya timu ya taifa ili kupata suluhisho.
“Nimefanya juhudi kurejesha michezo mashuleni, kurejesha UMISHUMTA na UMISETA. Nia yetu ni kuibua vipaj tangu shuleni na matumaini yetu ya usoni yatakuwa mazuri,”.
Rais Kikwete pia amesema wameingia ubia na taasisi ya Symbion Power na klabu ya Sunderland ya England kwa nia ya kuibua vipaji na tayari wamejenga kituo eneo la Kidongo Chekundu, Dar es Salaam kufundisha watoto wadogo.
“Tusikate tamaa, tuendelee kujitahidi na iko siku tutafanikiwa mbele ya safari, vituo vikiongezeka tutafika pale tunapokusudia,”amesema.
Rais Kikwete jioni ya leo amefunga Bunge ja Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi hapo Serikali mpya ya awamu ya tano itakapoingia madarakani.
Rais Kikwete, amemaliza awamu zake mbili za utawala tangu 2010 na sasa anasubiri Uchaguzi Mkuu mpya Oktoba mwaka huu akabidhi nchi kwa Rais mpya.

No comments: