MKURUGENZI wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers, Saed Kubenea pamoja na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Absalom Kibanda wameionya serikali juu ya uamuzi wa kulifuta gazeti la MAWIO uliochukuliwa hivi karibuni.
Kupitia tangazo la serikali lenye notisi namba 55, serikali ilichukua uamuzi wa kulifungia MAWIO, Januari 15, 2016 huku Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akisema gazeti hilo limekuwa ‘sugu’ kwa uchochezi tangu 2013.
Kubenea na Kibanda walikuwa katika kituo cha Polisi cha Kati ambapo ndiyo Makao Makuu ya Kanda Maalum ya Dar es Salaam wakiwasindikiza wahariri Jabir Idrissa na Simon Mkina walioitikia wito wa uliotolewa na jeshi hilo siku tatu zilizopita.
Kibanda amewambia wanahabari kuwa kitendo cha jeshi la polisi kuwasaka ili kuwakamata Jabir na Mkina ambao ni wahariri ili kuwahoji huku gazeti la MAWIO likiwa limefungiwa, kinalenga kuwatisha waandishi wa habari nchini na kuzima uhuru wa habari.
Ameulezea uamuzi huo wa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Habari, Nape, kama uamuzi uliolishitua TEF na wamewasiliana naye wakielezea mshituko na masikitiko yao.
“Hatuwezi kuvumilia kufungiwa kwa vyombo vya habari, kukamatwa na kunyanyaswa kwa waandishi, miaka miwili iliyopita nilitakiwa kujisalimisha makao makuu ya polisi, nikafikishwa mahakamani na nikashinda kesi, naelewa maumivu ya mapambano haya,” ameeleza Kibanda.
Kwa upande wake Kubenea, amesema Serikali kupitia Nape imechukua uamuzi wa kikatili dhidi ya gazeti la MAWIO ili kuzima sauti ya wananchi kwa hoja zisizo na mashiko ikiwemo ile ya uchochezi ambayo imekuwa kisingizio cha watawala kwa muda mrefu.
“Katika toleo la MAWIO lilimnukuu Maalim Seif akijitangaza mshindi, yeye hakuitwa mchochezi, Jecha amefuta uchaguzi wakati hana mamlaka ya kisheria wala ya kikatiba hakuitwa mchochezi ila gazeti kuandika ushindi uliotangazwa na Seif limefungiwa,”ameeleza Kubenea.
Kubenea ameongeza kuwa, ubovu wa sheria ya magazeti ya mwaka 1976 umekuwa ukitumiwa na serikali kuviadhibu vyombo vya habari vinavyofichua maovu, huku mahakama ikithibitisha mara kadhaa kuwa madai ya uchochezi yanayotolewa na serikali hayana mashiko.
“Jabir ni Mwandishi aliyebobea kitaaluma na uzoefu, ameandikia magazeti ya Uhuru, Mzalendo, Majira na New Habari huko kote hakuitwa mchochezi wala hakukamatwa.
“Nape alikuwa mmoja wa waandishi na vyanzo vya taarifa za MwanaHALISI kipindi hana madaraka CCM, mbona alishirikiana na sisi kuibua maovu kama sisi ni wachochezi?” alihoji Kubenea.
Jabir na Mkina wamekuwa wakitafutwa na jeshi la polisi kwa siku tatu mfululizo tangu Jumamosi kwa tuhuma za uchochezi huku jaribio la kuwakamata likishindikana mara kwa mara kutokana na kutojua walipo mpaka walipoamua kujisalimisha jana.
Mbali ya Kubenea na Kibanda, walisindikizwa pia na Mhariri Mtendaji wa gazeti la MwanaHALISI, Ansbert Ngurumo pamoja na wakili wao, Fredrick Kihwelo.
No comments:
Post a Comment