Friday 10 June 2016

Kilio Kwa watumia M-pesa, Tigo Pesa , Airtel Money na Wale wa Kwenye ATM.......Kila ukituma 1000/- utakatwa kodi 280/-


Wachambuzi na wadau mbalimbali wametoa maoni yao kuhusu Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17, huku watumiaji wa huduma za fedha kwa njia ya simu wakikumbwa na maumivu wa kodi.

Hiyo ni siku moja baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango kuwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 20116/17.

Pamoja na mambo mengine, bajeti hiyo inapendekeza kuongeza ushuru wa vinywaji baridi, maji ya juisi, vinywaji vikali, bia na sigara.

Pia itawagusa watumiaji wa M-pesa, Tigopesa, Airtel Money, Ezypesa   kwa kukatwa Sh 280 kwa kila Sh 1000 watakayotuma.

Jana Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), alisema hatua hiyo ya Serikali kuendelea kutafuta kodi kwa kuzidi kuwaumiza wananchi inakwenda kinyume na matarajio ya Watanzania wengi.

Alisema katika bajeti hiyo ya Serikali na ukusanyaji wa mapato yake, katika kila Sh  1000 itakayokatwa kwa huduma kwenye ATM kuanzia Julai Mosi mwaka huu, Sh 280 zitachukuliwa na TRA.

Zitto alisema hali hiyo pia itawakumba watumiaji wa miamala ya M-pesa, Tigopesa, Airtel Money, Ezypesa ambalo ndilo kundi kubwa la Watanzania wanaotumia huduma hiyo nchini.

Aawali kodi ya bidhaa ilikuwa asilimia 10 lakini kwa hatua ya kuongezwa kwa kodi ya ongezeko la thamani kodi itapaa na kufikia asilimia 28.

Kwa mantiki hiyo, katika kila Sh 100 kodi ni Sh 28 na  katika Sh 1000 kodi ni Sh 280.

Kutokana na hali hiyo kodi ya VAT hulipwa na mtumiaji wa mwisho ambaye anatuma au kupokea fedha, hali ambayo itawaumiza watumiaji wa mwisho.

“Hivyo hivyo katika miamala ya M-pesa, Tigo pesa na kadhalika, katika kila Sh 1000 itakayokatwa kwa huduma kwenye ATM kuanzia Julai 1, 2016, Sh  280 zitachukuliwa na TRA,” alisema Zitto.

Alisema   ameshangazwa na hatua ya Serikali kuongeza kodi ya VAT kwenye utalii hali ambayo inaweza kusababisha Tanzania kupoteza watalii wengi kwa washindani wake kwa sababu itaongeza gharama kwa watalii.

“Kama tunataka kutumia utalii kama kichocheo cha ajira ni vema kufikiria upya suala hili,”alisema.

Akizungumzia mapendekezo ya Serikali katika Sheria ya Kodi ya VAT ili kutoza kodi bidhaa zinazotoka Zanzibar, alisema hatua hiyo inavunja misingi iliyowekwa na sheria ya zamani ambayo ilifanana na ile za Zanzibar.

“Ikumbukwe kuwa Sheria ya Kodi ya VAT ya 2014 ilivunja misingi iliyowekwa ya sheria ya zamani ambayo ilifanana na ile ya Zanzibar. Mapendekezo ya sasa yana madhara makubwa kwa Zanzibar kwa sababu  hakuna atayewekeza Zanzibar ili kufaidika na soko la Bara.

“Biashara nyingi zinazozalisha Zanzibar zitahamia Tanzania Bara. Mapendekezo haya yanaweza kusababisha  mgogoro kati ya pande mbili za Muungano,” alisema.

No comments: