Wednesday 11 May 2016

Bomu la Mkono Laibua Hofu Tanga.....Ni baada ya Mtuhumiwa Kulirusha Baada ya Kukurupushwa na Polisi

Kwa mara nyingine jana wakazi wa Jiji la Tanga walikumbwa na taharuki baada ya kijana mmoja kurusha bomu la mkono chini ya daraja wakati wananchi walipokuwa wakimfukuza baada ya kukurupushwa na polisi.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Leonard Paulo alisema kijana huyo alikurupushwa na askari waliokuwa kwenye msako wa kuwatafuta majambazi waliofanya mauaji Aprili 20, mwaka huu katika duka la Central Bakery.

Alisema tukio hilo lilitokea juzi saa mbili usiku kwenye Mtaa wa Makora, Tarafa ya Ngamiani.

Awali, Kamanda Paulo alisema kijana huyo anayekadiriwa kuwa na miaka kati ya 25 na 30, alipokurupushwa alianza kutimua mbio. 

“Alipoanza kukimbia ndipo wananchi wakaingilia kati, walimfukuza na kumshambulia kwa mawe huku wakimpiga na kitu chenye ncha kali kisogoni, ndipo wakati akipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Tanga ya Bombo akafariki dunia njiani,” alisema Kamanda Paulo.

Mapema kabla hajafariki dunia, kamanda alisema kijana huyo alipokurupushwa alikimbia akiwa ameshikilia bomu mkononi.

Kamanda aliwataka wakazi wa Tanga kuwa watulivu kwa sababu vyombo vya dola viko katika operesheni maalumu ya kuwasaka walioshiriki mauaji ya hivi karibuni katika hilo la mikate.

Walioshuhuda tukio hilo walisema kijana huyo alishambuliwa na wananchi baada ya kukwapua simu ya mwanamke mmoja katika Mtaa wa Makorora.

No comments: