Wednesday 11 May 2016

Rais Magufuli: Huyu Shetani Aliyetulaani Watanzania kwanini Asife? Hivi Hatuhurumii hata Kidogo?

SHIRIKA la Taifa la Hifadhi za Jamii (NSSF) limetakiwa kuingia ubia na kampuni za madini nchini ili kutengeneza ajira kwa vijana wa Kitanzania ambao wengi wao wako vijiweni.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Rais John Magufuli wakati akizindua majengo ya mifuko ya pensheni ya NSSF na PPF yaliyogharimu zaidi ya Sh bilioni 60 yaliyojengwa jijini hapa.

Rais Magufuli alisema wakati umefika kwa NSSF kujikita katika biashara ya kupata faida kwa haraka kama vile ya madini ya tanzanite kwa kuanzisha viwanda vya kukata madini hayo na kusanifu ili vijana wafundishwe na hatimaye kuajiriwa katika viwanda hivyo.

Alisema suala la Tanzania kuwa nchi ya tatu duniani kwa kuuza madini ya tanzanite wakati madini hayo yanapatikana hapa hapa tu na kuziacha nchi za India na Kenya zikiongoza, ni suala la kushangaza sana.

Alisema NSSF sasa inapaswa kujipanga na kuingia katika biashara ya madini hususan tanzanite kwa kuingia ubia na kampuni kama hiyo ya Signature inayomilikiwa na mzawa Sailesh Pandit ili ifanye biashara na wanachama wa mfuko huo wapate faida haraka haraka na kuachana na uwekezaji wa majengo.

"Siku nyingine hakuna ubaya hata NSSF mkawa ndio wawekezaji wakubwa wa Tanzanite mkawa mnanunua Tanzanite kutoka kwa vijana hawa badala ya kuwa inavushwa mpaka Kenya na kwenda Kenya, badala ya Tanzania kuwa ya kwanza kuuza Tanzanite duniani inajitokeza India alafu inafata Kenya

"Unajua saa nyingine watu wanatuona Watanzania sijui tukoje, huyu shetani aliyetulaani sisi Watanzania kwanini asife? hata hatuhurumii kidogo? basi kama ni kuswali na kusali tusali sana ili tubadilike, tuthamini mali yetu kwa ajili ya vizazi vyetu." Alisema RAais Magufuli

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alisema kampuni ya madini ya Signature iliyopanga katika jengo la mfuko huo la Mafao House imeajiri vijana zaidi ya 47 wa kuchonga tanzanite na watashirikiana katika kuanza biashara hiyo.

Profesa Kahyarara alisema kauli ya Rais ya shirika hilo kujikitaka katika biashara ya tanzanite kwa kuanzisha viwanda vya kuchonga madini hayo wataifanyia kazi haraka iwezekanavyo bila ya wasiwasi wowote.

Hata hivyo, serikali ilishapiga marufuku usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi na kutaka madini yote kuchongwa nchini na wazawa kuanzisha viwanda vya kuchonga madini hayo.

No comments: