Wanachama
wanaotaka kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM, sasa watalazimika kuwa
wakazi wa eneo wanalotaka kuliwakilisha, sharti ambalo linaweza
kuwaondoa takriban nusu ya wabunge wa sasa.
Kutokana
na Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuruhusu mtu kwenda sehemu yoyote
apendayo, imekuwa rahisi kwa mtu kuishi mji kama Dar es Salaam na
kugombea ubunge wa jimbo lililoko katika mkoa mwingine.
Na
uhuru huo umewawezesha watu kama Augustine Mrema, ambaye ni mwenyekiti
wa chama cha TLP, kuwa mbunge wa Moshi Vijijini kwa tiketi ya CCM,
Temeke (NCCR-Mageuzi) na Vunjo (TLP).
Na
ni kutokana na uhuru huo, wabunge wengi wa vyama tofauti, wanaishi Dar
es Salaam na kuwakilisha majimbo ya maeneo ya asili yao.
Hata
wafanyakazi kutoka serikalini, hasa wakuu wa mikoa na wilaya na sehemu
nyingine, huchukua likizo wakati wa uteuzi wa wagombea na kwenda maeneo
yao asilia au waliyokulia kuomba wapitishwe na wasipopitishwa hurejea
makazini.
Lakini
masharti mapya ya CCM yanazuia mwanachama kugombea ubunge, udiwani au
nafasi nyingine yoyote bila ya kuwa mkazi wa eneo hilo.
“Shika
maneno yangu, mwaka 2020 wagombea ubunge watakuwa ni wale ambao
wanatoka kwenye maeneo husika, wanaojua na kushughulika na shida za
wananchi,” alisema katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole
katika mahojiano na kituo cha redio cha Times FM jana.
Alisema
hatua hiyo imetokana na chama hicho kujitathmini na kujisahihisha baada
ya kugundua watu wanataka viongozi wanaotoka miongoni mwao ambao
wanajua kero zao na hivyo wataweza kuzishughulikia.
Polepole,
ambaye alipata umaarufu wakati wa Bunge la Katiba akitaka litumie
rasimu iliyotokana na maoni ya wananchi, alisema wanachama watakaokuwa
wakazi wa maeneo tofauti na wanayotaka kuyaongoza, hawataruhusiwa.
Akihojiwa
katika kipindi cha Maisha Mseto, Polepole alisema ili mwanaCCM awe na
sifa za kugombea, ni lazima awe mkazi wa eneo husika.
Polepole,
ambaye alikuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na
Jaji Joseph Warioba, alisema suala hilo lilikuwa sehemu ya maoni ya
wananchi wakati wa mchakato wa Katiba Mpya.
Alisema msisitizo mkubwa uliopo ni cheo kimoja kwa mtu mmoja jambo linalofundisha kuwa watu wenye kiasi.
“Haya
mambo ndiyo watu wanayoyataka. Rais (John) Magufuli alienda mbele zaidi
kwamba utagombea nafasi ya uongozi kwenye eneo ambalo wewe ni mkazi
vinginevyo, marufuku kugombea,” alisema Polepole.
“Mwaka 2020 unakuja, si mtu upo zako Times FM unapiga kazi, halafu ikifika mwishoni unaenda Ileje eti unaenda kuchukua jimbo.”
Akizungumzia
uamuzi huo, katibu wa wabunge wa CCM, Jason Rweikiza alisema sharti
hilo litakomesha tabia iliyojengeka kwa baadhi ya wanachama wa chama
hicho kwenda kugombea ubunge maeneo ambayo hawajui yana matatizo gani.
“Unakuta
wananchi wana shida ya maji, umeme na barabara anakuja mgombea kipindi
cha uchaguzi na ahadi kemkem, kumbe yote ni kuwavutia wampigie kura na
akishajihakikishia ushindi humumuoni tena,” alisema Rweikiza.
Rweikiza
alisema hatua hiyo itasababisha watu wathamini kwao na kuelewa matatizo
ya maeneo waliyotoka na uchaguzi utakuwa huru bila ya rushwa.
No comments:
Post a Comment