Serikali
imeeleza kwamba matatizo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HESLB) ni kulipwa kwa wanafunzi hewa, ubadhirifu wa fedha na kuwepo
kwa watendaji wanaohusika kuweka fedha za wanafunzi wanne kwa mwanafunzi
mmoja.
Kadhalika
imeeleza tabia ya HESLB kujiona ‘Mungumtu’, kuwaona watoto wa
Watanzania kama ni shida kwao na wasiostahili kupewa mikopo na hata kuwa
na majibu ya mkato yasiyokuwa na chembe ya kazi ya utoaji huduma.
Waziri
wa Elimu, Sayansi ya Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema hayo
jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua Bodi mpya ya HESLB na
kuitaka kujitenga na menejimenti wakati wa utekelezaji wa majukumu yake
na kuhakikisha matatizo hayo yote ambayo yapo katika taarifa
aliyowakabidhi, yanakaguliwa upya, kuhakikiwa na kufanyiwa kazi.
Alikabidhi
taarifa hiyo kwa Makamu Mwenyekiti wa bodi mpya, Madina Mwinyi akiagiza
ifanyiwe kazi kuhakikisha na kujiridhisha pamoja na kuwajua wadeni wa
HESLB huku ikiepuka kuiamini menejimenti kama ilivyokuwa kwa bodi ya
awali badala yake kuisimamia.
“Ninakabidhi
taarifa yenye changamoto za Bodi ya Mikopo kwenu Bodi ya Wakurugenzi
ambayo inaainisha uwepo wa wanafunzi hewa na ambao wanalipwa mikopo
wakiwemo waliomaliza au kuacha chuo,” alisema.
Pia
alisema taarifa hiyo inahusisha kuwepo kwa watendaji wanaohitajika
kujieleza ambao walikuwa wakiweka fedha za wanafunzi wanne kwa
mwanafunzi mmoja ambapo ushahidi upo na eneo hilo bado kuna shida.
Kadhalika,
aliiagiza Bodi mpya kutazama upya na kujiridhisha kuhusu vigezo vya
utoaji mikopo kwani kumekuwa na matatizo, na hata kutizama utoaji wa
mikopo kama taratibu na sheria zinazingatiwa.
“Malalamiko
ya Bodi ya Mikopo yapunguzwe ama kuondolewa kabisa ili kukidhi
matarajio ya wadau wa elimu nchini, endeleeni kukagua na hata majina ya
wanaohitajika kupata mikopo kabla ya kutolewa rasmi,” alisema Profesa
Ndalichako.
Kuhusu
Bodi mpya aliitaka isimamie zaidi urejeshwaji wa mikopo kwani hadi sasa
serikali imetoa Sh trilioni 3.1 tangu kuanzishwa kwa bodi, lakini ni Sh
milioni 217 pekee zilizorejeshwa huku Sh bilioni 588 zikiwa zimefikia
muda wake zikitakiwa kulipwa.
Akizungumza
baada ya bodi hiyo kuzinduliwa, Makamu Mwenyekiti, Madina Mwinyi
alisema katika kufanyia kazi changamoto za HESLB wataanza kwa kujipanga
wao wenyewe katika taasisi wanamotoka ili kila mmoja kujua ni kiwango
gani cha mikopo kinachotakiwa kurejeshwa.
Kadhalika
alisema bodi hiyo itahuisha taswira ya HESLB pamoja na kuiaminisha
jamii kuwa suala la mkopo wa elimu ya juu ni lazima kurejeshwa kwa
wakati.
Wajumbe
wa bodi hiyo na taasisi wanazotoka katika mabano ni Profesa Caroline
Nondo (Mwakilishi kutoka Tume ya Vyuo Vikuu), Susan Urio (Mwakilishi wa
Wanafunzi), Madina Mwinyi ambaye ni Makamu Mwenyekiti (Mwakilishi wa
Wizara ya Elimu Zanzibar).
Wengine
ni pamoja na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Gerson Mdemu
(Mwakilishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali), Dk Dalmas Nyaoro
(Mwakilishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia), Frank Mgeta
(Mwakilishi wa Wizara ya Fedha na Mipango), Dk Francis Masika
(Mwakilishi wa Baraza la Elimu ya Ufundi) na Mjumbe mmoja ambaye ni
Mwakilishi wa Wizara ya Fedha Zanzibar hajateuliwa.
No comments:
Post a Comment