Wednesday 4 October 2017

WIZARA YA AFYA YATOA TAHADHARI KUHUSU UGONJWA WA TAUNI ULIOATHIRI NCHI YA MADAGASCAR



Image result for ummy mwalimu
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inapenda kutoa taarifa kwa umma, kuhusu kuwepo ugonjwa wa tauni katika nchi ya Madagascar kuanzia Agosti, 2017. Taarifa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) imeeleza kuwa nchini Madagascar mikoa minane (8) imeripoti kupata wagonjwa ikiwa ni pamoja na Antananarivo ambao ni Mji mkuu wa Madagascar, Sava, Tamatave/Atsinanana na Majunga /Boeny. Kati ya Agosti 23 hadi Septemba 28 mwaka huu, wagonjwa 104 wameripotiwa na kati yao ishirini (20) wamepoteza maisha (CFR 19.2%).
Wagonjwa wengi walioripotiwa wameonyesha kuwa na uhusiano kwa njia moja au nyingine na mgonjwa wa kwanza, jambo linalothibitisha kuwa yapo maambukizi ya ugonjwa wa tauni kati ya binadamu na binadamu. Hivyo, kwa mujibu wa WHO, upo uwezekano wa kadri (moderate risk) wa ugonjwa huo kusambaa katika nchi jirani na Madagscar.
Tahadhari hii inatolewa kwa kuzingatia kwamba nchi ya Madagascar haiko mbali sana na Tanzania, na inawezekana kukawa na muingiliano kati ya wananchi wa Tanzania na wale wa Madgascar. Inasisitizwa kwamba kwa sasa hapa nchini Tanzania hakuna mgonjwa yeyote aliyeripotiwa.
UGONJWA WA TAUNI
Ugonjwa huu unasababishwa na bakteria anayejulikana kitaalam kama “Yersinia pestis”, ambaye hupatikana katika baadhi ya wanyama wadogo kama vile panya, paka na mbwa na viroboto. Ziko njia kuu tatu ambazo mtu anaweza kupata maambukizi:

  1. Kung’atwa na viroboto vyenye maambukizi ya bakteria hao kutoka kwa wanyama kama mbwa na paka ambao huweza kubeba viroboto hawa.
  2. Kugusana bila kuwa na vikinga mwili na majimaji yenye vimelea vya bakteria kutoka kwa mtu/mnyama aliyeathirika kwa njia ya kugusa sehemu zenye vimelea zilizochafuliwa na mgonjwa/mnyama na kasha mtu huyo kujigusa mdomomi au puani.
  3. Kugusana na majimaji yanayotoka kwa mgonjwa kwa njia ya kukohoa au kupiga chafya bila ya mgonjwa huyo kufunika pua au mdomo.
Ugonjwa wa tauni hujitokeza kwa aina kuu tatu:
  1. Kuathiri mitoki (Bubonic plague):
Mgonjwa hupata homa, kusikia baridi, mwili kukosa nguvu na mitoki kuvimba katika makwapa na mapaja. Mgonjwa asipotibiwa ugonjwa husambaa sehemu nyingine za mwili. Aina hii hutokea baada ya mtu  kuumwa na viroboto au kuhudumia mnyama aliyeathirika.
  1. Maambukizi katika damu (Septicemic plague)
Mgonjwa hupata homa, kusikia baridi, mwili kukosa nguvu kabisa, maumivu ya tumbo, ngozi kuvia damu pamoja na viungo vingine. Aina hii hupatikana kwa kuumwa na viroboto au kuhudumia mnyama aliyeathirika.
  1. Tauni inayoathiri mfumo wa hewa (Pneumonic plague):
Mgonjwa hupata homa, kichwa kuuma, mwili kuishiwa nguvu na kupata kichomi (nimonia) kikali na kupumua kwa shida. Pia hukohoa na kupata maumivu ya kifua. Hii huambukizwa kwa kuvuta hewa au majimaji ya mfumo wa hewa kutoka kwa mgonjwa, au endapo aina mbili za hapo juu hazikutibiwa kikamilifu na vimelea vikashambulia mapafu. Aina hii ni hatari sana na ni aina pekee inayoweza kuambukizwa toka kwa binadamu aliyeambukizwa kwenda kwa mwingine. Aina hii ndiyo imethibitishwa kuwepo huko Madagascar kwa wakati huu.
Kwa bahati nzuri ugonjwa wa Tauni unatibika hivyo ni muhimu kuwahi katika vituo vya kutolea huduma ya afya mara mtu anapoona dalili.
HATUA ZINAZOCHUKULIWA NA WIZARA KATIKA KUZUIA UGONJWA HUU USIINGIE NCHINI
Hatua zifuatazo zimechukuliwa baada ya kupata taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu  kutoka WHO hapo Septemba 29, 2017;
  • Kuandaa barua za tahadhari za ugonjwa huu kwa Makatibu Tawala wa mikoa yote ya Tanzania Bara kwa ajili ya kuwataarifu na kuwataka kuchukua tahadhari.
  • Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa katika viwanja vya ndege, mipakani pamoja na bandari ili kubaini wagonjwa waingiao nchini wakiwa na dalili za ugonjwa huo.
  • Kupitia kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wizara inatoa maelekezo ya kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na utambuzi wa magonjwa (Surveillance) katika vituo vya kutolea huduma nchini kote.
  • Wizara itatoa elimu kwa jamii kuhusu ugonjwa huu.
Ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu jamii inaaswa kuzingatia yafuatayo:
  1. Kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za afya mara wanapoona dalili.
  2. Kuimarisha usafi wa mazingira.
  3. Kudhibiti viroboto kwa dawa.
  4. Kudhibiti panya katika makazi yetu.
  5. Mazao yahifadhiwe vizuri kuepuka kuwavutia panya kuja katika makazi yetu.
  6. Wanyama waogeshwe kama inavyoelekezwa na wataalam wa mifugo ili kuepuka viroboto ambavyo hubeba vimelea vya tauni.
  7.  Kuacha utaratibu wa Binadamu kukaa nyumba moja na wanyama.
Hitimsho
Serikali inasisitiza kuwa mpaka sasa ugonjwa wa tauni haujaingia hapa nchini. Kwa kuwa magonjwa hayaangalii mipaka, tunahitaji kuchukua tahadharii madhubuti ili kuzuia ugonjwa huu usiingie hapa nchini. Hivyo wananchi wanahimizwa kuzingatia kanuni za afya za kuzuia ugonjwa huu, pia wanatakiwa kuripoti haraka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mara waonapo dalili zozote za ugonjwa huu.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Afya
03 Oktoba, 2017

No comments: