Juhudi
za kuudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu Wilayani Kyela huenda ukagonga
mwamba kutokana na milundikano ya taka ngumu kuongezeka
siku hadi siku kama inavyoonekana katika picha zikionesha ndani na nje
ya soko kuu huku kukiwa na hofu kuwa ugonjwa huo utazidi kuenea kama
juhudi za haraka hazitachukuliwa.
MBALI na maambukizi ya
Ugonjwa wa Kipindupindu kushika kasi Wilayani Kyela Mbeya kutoka wagonjwa 39 wiki iliyopita hadi kufikia
wagonjwa 75 kwa takwimu za jana hali ya mazingira ndani ya Wilaya hiyo hasa Mamlaka
ya Mji mdogo wa Kyela wazidi kuwa mchafu kutokana na kukithiri kwa mlundikano
wa taka ngumu kuzidi kuongezeka siku
hadi siku.
Baadhi ya wakazi wa mji
wa Kyela wametoa malalamiko hayo jana kwa Afisa mtendaji mkuu wa mamlaka ya mji
mdogo baada ya kuona hali ni tete kutokana na kuongezeka kwa ugonjwa wa kipindupindu huku Serikali
ikishindwa kuuweka mji wa Kyela katika hali ya usafi kitu ambacho kinawapa hofu
juu ya kuudhibiti ugonjwa huo.
Wafanyabiashara katika
soko kuu la Kyela kwa upande wao wameshangazwa na kitendo cha mamlaka hiyo ya
mji mdogo kushindwa kutoa taka ngumu
zilizojaa kila kona ya soko na nje ya soko hilo bila kuziondoa huku wakiendelea
kutozwa ushuru.
Wamewataka viongozi hao
kuondoa taka hizo ili kurudisha hadhi ya mji wa Kyela na wao waweze kuona fedha
zao wanazozitoa kwa ajili ya ushuru wa uzoaji wa taka ngumu ukifanya kazi.
Afisa mtendaji mkuu wa
mamlaka ya mji wa kyela Teo Samwel mbali na kukiri kuwepo na hali hiyo pia
alisema kuwa tatizo ni gali linalotumika kubeba taka limeharibika na lipo
katika matengenezo wataziondoa taka hizo pindi matengenezo ya gali hilo
yatakapokamilika.
Naye Mganga mkuu wa Wilaya ya Kyela Apasalia
Lumisha alitaja ongezeko la wagonjwa wa Kipindupindu kuwa ni 75 mpaka hivi sasa
na waliopoteza maisha kufuatia kukumbwa na ugonjwa huo ni watu watatu.
Alisema kuwa kufuatia
hali hiyo halmashauri ya wilaya imetenga eneo la uwanja wa Mwakangale mjini
Kyela na kujenga mahema matano ya kuanzia kama kambi kuu ya kuhifadhi wagonjwa
hao wa kipindupindu na kuwa wote waliolazwa katika hospitali ya wilaya
watahamishiwa katika uwanja huo.
Alisema kuwa bado jamii
inapuuzia juu ya mlipuko huo wa kipindupindu na ndiyo maana kasi hiyo
imeendelea na kuwa anakazia amri yake aliyoitoa juzi ya kukataza mikusanyiko
mbalimbali ya watu isiyo rasmi,minada na sherehe mbalimbali sambamba na
biashara ya vyakula na vilabu vyote vinavyouza pombe za kienyeji
Pia mkuu huyo wa wilaya
ameagiza wafanyabiashara kuacha kupeleka biashara ya vyakula katika shule zote
za msingi na sekondari kwa kipindi hiki ambacho shule zimefunguliwa mpaka pale
watakapo tangaziwa na kupewa ruhusa.
Ugonjwa huo wa
kipindupindu umezidi kuenea maeneo mbalimbali ya wilaya Kyela ambapo awali kata
sita za Kajunjumele,Bujonde,Ikolo,Katumbasongwe
na Kyela mjini ndizo zilikuwa na wagonjwa hao lakini sasa hata kata ya Ipande
mgonjwa mmoja ametambulika na kupoteza maisha.
Aliongeza kuwa
kumekuwepo na ugumu kwa wananchi kupokea ushauri kuhusu nanma ya kujikinga na
ugonjwa huo ambao unakwepeka na kuwa bado wanaendelea kutembelea kila Kata
ndani ya wilaya ili kuzidi kutoa elimu na namna ya kujikunga na
maambukizi ya ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kugawa dawa za kutibu maji (Water
guard).
Na Ibrahim Yassin, Kyela
No comments:
Post a Comment