Friday, 11 January 2013

Viongozi wa Jumuia ya Maendeleo kusini mwa Afrika wakutana Dar es Salaam, kujadili Mgogoro wa Congo


Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete
Rais wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete

Viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa afrika SADC wanakutana jijini Dar es Salaam nchini Tanzania hii leo kwenye mkutano unaotarajiwa kutawaliwa na ajenda kuhusu mgogoro wa mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya kongo DRC na nchi ya Madagascar.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Tanzania, Ally Kombo amethibitisha kufanyika kwa mkutano huo na kuongeza kuwa suala la mgogoro wa mashariki mwa DRC na ule mgogoro wa Madagascar ndio zitakuwa ajenda kuu za mkutano huu wa mwisho nchini Tanzania.

Juma moja lililopita mkuu wa masuala ya usalama kwenye Umoja wa Afrika Ramtane Lamamra alisema nchi ya Tanzania itapeleka kikosi cha wanajeshi mashariki mwa nchi hiyo kulinda usalama na kufanya tathimini.

Mkutano huu utahudhuriwa pia na rais wa Afrika Kusini Jackob Zuma, rais wa Namibia Hifikepunye Pohamba pamoja na rais wa msumbiji Armando Guebuza ambapo pamoja na mambo mengine wanatarajiwa kuzungumzia masuala ya usalama kwenye ukanda wao na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Zimbabwe.

Katika hatua nyingine mpango wa kusaidia majeshi ya kulinda amani nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kutumia ndege maalum za upelelezi umeungwa mkono na Marekani, licha ya upinzani kutoka Rwanda na Majirani wengine.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani Victoria Nuland amesema kuwa Ndege hizo zenye vifaa vya kunasa picha pia zinaweza kutumika pia katika nchi nyingine lakini ikiwa nchi hizo zitaridhia lakini akataadharisha kuwa hazitaingilia uhuru wa nchi husika.


Ndege hizo zimeelezwa kuwa na lengo la kulinda Raia na kusaidia Congo katika kustawisha usalama wa nchi.

No comments: