Wednesday 21 February 2018

IFISI HOSPITAL FC YAICHOMA SYUKULA 2-0

NA GORDON KALULUNGA, MBEYA

KATIKA Uga wa Sokoine Jijini Mbeya leo, timu ya Ifisi Hospital FC imeigagadua goli mbili kwa nunge timu ya Syukula katika ligi ya daraja la Tatu mkoa wa Mbeya ngazi ya Sita bora huku timu ya Tukuyu Stars ikiifunga goli 3-2 timu ya Iduda FC.

Dakika ya 5 ya kipindi cha kwanza, mchezaji Frank Kavila wa timu ya Ifisi Hospital alifanya kashikashi ya kutisha katika lango la Syukula FC hatimaye mpira ukajaa wavuni na kuiandikia timu ya Ifisi goli la kwanza.

Mchezaji huyo Frank Kavila, aliwaamsha tena mashabiki wa timu hiyo dakika ya 28 baada ya kutikisa nyavu za Syukula FC kwa shuti lililonyoka vema na kuiandikia timu yake goli la pili mpaka kipindi cha kwanza kuisha, Ifisi ikaongoza gali mbili kwa sifuri.

Kipindi cha pili timu ya Syukula ilibadili mchezo wake na kuuweka mpira chini tofauti na kipindi cha kwanza ambapo walileta ushindani mkubwa lakini mpaka mpira unamalizika Ifisi ikaibuka na pointi 3 za muhimu na kufikisha pointi 10 ambapo inatarajia kuchuana na timu ya Tukuyu Stars hapo Februari 25, mwaka huu huku Tukuyu Stars ikiwa na pointi 9.

Baada ya mchezo kumalizika katika uwanja wa Sokoine, uongozi wa timu ya Syukula uligoma kuzungumza na waandishi wa habari huku uongozi wa Ifisi Hospital ukisema kuwa mchezo wa soka hauhitaji hasira.

Katibu wa timu ya Ifisi Hospital Chris Nathaniel alisema kuwa mchezo ulikuwa mgumu lakini wao wanashukuru kwa kuibuka washindi na kuwaomba wadau waungane katika kuipa nguvu timu hiyo hasa kipindi hiki inapoelekea kukipiga na timu kongwe ya Tukuyu Stars na kwamba wao wanaleta mapinduzi katika soka la mkoa wa Mbeya.

Kwa upande wake Katibu wa Hospitali ya Mbalizi Ifisi Emmanuel Martin, alisema kuwa amefurahishwa na kiwango walichoonyesha wachezaji wa timu hiyo na kwamba wamewapa moyo mkubwa na sasa wanatazamia kuibuka washindi katika mechi kati yao na Tukuyu Stars.

“Tunawatumia salamu ndugu zetu Tukuyu Stars kuwa wajipange vema maana tunaenda kuchukua ubingwa nyumbani kwao na sisi magoli yetu ni kuanzia matano na ninawapongeza sana waamuzi kwa kuchezesha vizuri na ninaamini watamaliza vizuri katika mechi yetu na Tukuyu Stars. Haya maneno ya kusema tutahujumiwa naomba mashabiki wa timu yetu wayapuuze. Tutawachoma sindano za kutosha Tukuyu” alisema Katibu huyo.

No comments: