Tanesco yaanza kutekeleza bei mpya za kuunganisha umeme
Shirikala
Umeme Tanzania (Tanesco) limeanza kutekeleza bei mpya za kuunganisha
umeme zilizotangazwa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter
Muhongo, kwamba, zingeanza kutumika mwezi huu. Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, mmoja wa maofisa wa Tanesco
Wilaya ya Ilala, alisema kuanzia mwezi huu wameanza kutoza Sh. 320,960
badala ya Sh. 455,000 za hapo awali kwa wateja wanaounganisha umeme moja
kwa moja bila kutumia nguzo kwa umbali usiozidi mita 30 mijini.
Alisema
kwa wateja wanaohitaji kuunganishiwa umeme kwa njia moja kwa kutumia
nguzo moja, wanatozwa Sh. 515,618 badala ya bei ya awali ya Sh.
1,351,884 za awali.
Ofisa huyo, ambaye hakutaka kutaja jina lake kwa kuwa si msemaji wa
shirika hilo, alisema kwa upande wa wateja wanaounganishiwa umeme kwa
njia moja na nguzo mbili hutozwa Sh. 454,6454 badala ya Sh. 696,670 za
awali.
Katika hotuba yake ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa
2012/2013, aliyoitoa bungeni, mwaka jana, mjini Dodoma, Waziri Muhongo
alisema wizara yake kupitia Tanesco imedhamiria kupunguza gharama za
kuunganisha umeme.
Alisema dhamira hiyo inalenga kutimimiza malengo ya serikali ya kuongeza
idadi ya Watanzania wanaotumia nishati hiyo kote nchini kutoka asilimia
18 ya sasa hadi asilimia 30 ifikapo mwaka 2015.
Pia akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mpango huo mwaka
jana, Waziri Muhongo aliwahakikishia Watanzania kuwa ifikapo Januari,
mwaka huu, wataanza kuunganishiwa nishati hiyo kulingana na gharama za
punguzo zilizopangwa na serikali kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mijini
na vijijini.
Kwa mujibu wa punguzo hilo, wateja watakaojengewa njia moja katika
umbali usiozidi mita 30 bila kuhitaji nguzo kwa maeneo ya vijijini,
wataunganishwa kwa Sh. 177,000 kutoka ile ya zamani Sh. 455,000 sawa na
punguzo la asilimia 61.11 wakati kwa upande wa mijini ni Sh. 320,960
kutoka Sh. 455, 000, ambayo ni sawa na punguzo la asilimia 29.48.
Njia moja na nguzo moja kwa upande wa vijijini, wataunganishiwa kwa Sh.
337,740 kutoka ile ya zamani Sh. 1, 351,884 sawa na punguzo la asilimia
75.02 na mijini 515,618 kutoka ile ya zamani Sh. 1, 351,884 sawa na
punguzo la asilimia 61.86.
Kwa watakaohitaji kuunganishiwa umeme wa njia moja na nguzo mbili,
watalipa Sh. 454,654 kwa wale wa vijijini ni Sh. 696, 670 kwa wale wa
mijini, gharama ambazo kwa mujibu wa Wizara ya Nishati Madini, zitaanza
kutumika rasmi kuanzia mwezi huu.
Waziri Muhongo alisema matarajio ya kupunguziwa gharama hizo
yanakabiliwa na ukinzani mkubwa baada ya Tanesco kutoa maombi ya
kupandisha gharama za umeme kwa asilimia 81.27 ili kufidia hasara ya
takriban Sh. bilioni 160 kutokana na gharama za matumizi zinazokadiriwa
kufikia Sh. bilioni 250 kuzidi mapato yanayoingizwa katika shirika hilo
ya Sh. bilioni 90 kila mwezi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment