Mchakato wa KATIBA:Mtikila aibua mapya
MAKUNDI
maalumu jana yaliendelea kutoa maoni yao kwenye mchakato wa Katiba Mpya,
huku DP kikipendekeza Rais aapishwe baada ya siku 90 tangu kumalizika
kwa Uchaguzi Mkuu. Mbali
na maoni hayo yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Mchungaji
Christopher Mtikila, makundi mengine; wakulima, wafugaji, wanahabari na
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) nayo yalijitokeza kutoa moyoni.
Mtikila
alisema kipindi hicho cha siku 90 kitatoa fursa kwa watu wanaotaka
kuwasilisha pingamizi dhidi ya ushindi wa Rais mteule kufanya hivyo,
kabla ya kuapishwa.
Alisema
pingamizi linaweza kufanyiwa kazi kwa kipindi hicho cha miezi mitatu
ili kuhakikisha kuwa taifa linapata kiongozi halali mwenye ridhaa ya
wananchi.
“Pia
tunataka kinga ya Rais ikome pale anapomaliza muda wake wa uongozi, kama
alifanya makosa yoyote ya jinai aweze kushtakiwa ili kujenga nidhamu ya
uongozi katika ofisi ya umma. Utaratibu wa kumwondoa madarakani
uimarishwe asisubiriwe hadi amalize muda wake wa uongozi.”
Alisema kuwa
Katiba ya nchi inapaswa kuwa mali ya wananchi wenyewe ili watawala
wasijihusishe katika kuwaundia wananchi Katiba kama ilivyo kwa mchakato
unaoendelea sasa wa kupata Katiba Mpya.
“Kumekuwa na
hoja ya kuwapo kwa Serikali ya Tanganyika, hilo ni jambo muhimu na watu
kutoka Tanganyika ni lazima wawe na Serikali yao ndani ya mipaka ya
ardhi yao kupitia Katiba Mpya,” alisisitiza Mchungaji Mtikila.
Aliongeza
kuwa nafasi za wabunge wa viti maalumu bungeni ziondolewe ili viti hivyo
vishindaniwe kidemokrasia. Alisema wanawake wanatakiwa waelimishwe na
kupikwa ili wahimili ushindani katika medani za kisiasa. Alisema kuwa
taifa linahitaji viongozi bora na siyo kustarehesha jinsia.
Jukwaa la Wahariri
Jukwaa
la Wahariri Tanzania (TEF) limependekeza Katiba ijayo kutambua uhuru wa
vyombo vya habari, haki ya kupata habari na uhuru wa kutoa mawazo.
“Kwa
Katiba hii na sheria nyingine yoyote isiyoendana na Katiba hii, milele
haitaruhusiwa kudhibiti habari nchini Tanzania,” ilieleza taarifa hiyo.
TEF ilisema
kuwa haitakiwi kuwe na vikwazo katika kuanzisha magazeti au vyombo vya
habari binafsi, kwamba wahariri na wachapishaji wa magazeti na vyombo
vingine vya habari hawatakiwi kudhibitiwa au kuingiliwa na Serikali.
“Chombo
chochote cha habari chenye wajibu wa kusambaza taarifa kwa jamii ambacho
kinachapisha taarifa kuhusu, au dhidi ya mtu yeyote kinawajibika kutoa
fursa ya kuchapisha mawazo ya upande wa pili, ikiwa yapo, kutoka kwa mtu
ambaye taarifa au chapisho linamhusu,” ilieleza taarifa hiyo.
Vilevile,
wamependekeza kuwe na sheria ya Bunge ya kuanzisha Baraza la Habari la
Taifa, ndani ya miezi sita tangu siku ya kuanza kutumika kwa Katiba
Mpya, baraza ambalo litakuwa na wajumbe 15 kutoka katika taaluma
mbalimbali.
“Wajibu wa
Baraza la Habari la Taifa itakuwa ni kusimamia vyombo vya habari, kuweka
viwango vya kitaaluma kwa vyombo vya habari, kufuatilia utekelezaji wa
viwango vilivyowekwa, kukuza taaluma na weledi katika vyombo vya
habari,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza; “Kusikiliza
mashauri au malalamiko dhidi ya vyombo vya habari, gharama za
uendeshaji wa baraza. Kwa mujibu wa Katiba hii, Baraza la Habari la
Taifa ndicho kitakuwa chombo cha mwisho katika kusimamia tasnia ya
habari nchini.”
Katika
suala la haki ya kupata habari, TEF imesema kila mwananchi ana haki ya
kupata taarifa zozote hata zile zilizopo mikononi mwa Serikali.
Katika
suala la uhuru wa kutoa mawazo Jukwaa hilo limeeleza kwamba kila mtu
ana uhuru wa mawazo unaohusisha uhuru wa kutafuta, kupokea au kutoa
taarifa au mawazo.
Baraza hilo
limesema kuwa uhuru huo hautahusisha propaganda kwa ajili ya vita,
uchochezi wa kuanzisha vurugu, hotuba za chuki, utetezi wa chuki,
ukabila, ubaguzi kwa watu wengine au kuchochea mapambano.
No comments:
Post a Comment